Utumizi Wa Lugha
How to register and join MyElimu CLICK HERE

Post Reply 
 
Thread Rating:
  • 0 Votes - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
Utumizi Wa Lugha
MwlMaeda Offline
Teacher
Teacher

Posts: 41
Likes Given: 1
Likes Received: 3 in 3 posts
Joined: Feb 2017
Reputation: 0
Friend:  Add as Friend

Points: 3,446.38 points
Country: Tanzania
Post: #1
Utumizi Wa Lugha

0
0
UTUMIZI WA LUGHA
Dhanna ya utumizi wa lugha na mambo ya kuzingatia
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi.
Matumizi ya lugha ni maarifa yanayokusudiwa kumpa msomaji ujuzi utakaomwezesha:
- Kuitumia lugha yake kwa usanifu na ufasaha awapo katika mazingira tofauti tofauti
- Kumwezesha mtumiaji lugha kutambua, kutofautisha na kutumia mitindo mbalimbali ya lugha
- Kubaini makosa mbalimbali yanayofanywa na watumiaji wa lugha na kuyasahihisha
Dhima ya matumizi ya lugha
Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii inayohusika.
(a) Mada (Nini?)
Mada za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii, kwa mafano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k. Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara, faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.

(b) Madhumuni (Kwa nini?)
Malengo ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya lugha. Kwa mfano, lengo linaweza kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia moyo n.k. Sasa jinsi lugha itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti na itakavyotumika katika kutia moyo au kukejeli.

© Uhusiano (Nani?)
Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi, marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi, mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili yatategemea uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa.

(d) Utanzu wa mawasiliano (Kwa vipi?)
Hii ni njia ambayo mtu huitumia kufikisha ujumbe wake. Jinsi ya kutumia lugha na namna ya kuwasilisha ujumbe hutegemea sana uhusiano baina ya mzungumzaji na yule anayezungumzishwa. Mathalan, unaweza kutumia mazungumzo ya mdomo ana kwa ana, mazungumzo kwa njia ya simu au njia ya maandishi.
(e) Muktadha (Wapi?)
Mazungumzo yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa mfano kuna miktadha ya kidini, kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu, kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza kufanyika mjini, kijijini, ugenini, shuleni, dukani, hotelini n.k

MITINDO MBALIMBALI YA LUGHA
1. Mtindo wa kitaaluma
Mtindo huu unatumiwa katika mazungumzo na maandishi ya kitaaluma. Miktadha ya mazungumzo ya kitaaluma ni kama vile kwenye semina na makongamano ya kitaaluma na katika utoaji wa mafunzo kwenye shule na vyuo.

Mtindo wa kitaaluma hutawaliwa na sifa zifuatazo:
(i) Matumizi makubwa ya istilahi ya lugha husika mf. Isimu, mofimu, nomino, kishazi, n.k
(ii) Matumizi ya maneno ya kigeni ya kimataifa mf. Haidroksaidi, leksikografia, nyukilia, n.k
(iii) Matumizi makubwa ya wakati uliopo na hali ya mazoea mf. Mwandishi anazunguzia kuhusu umaskini…..
(iv) Matumizi ya nafsi ya tatu mf. Kikao kiliamua kuwa uteuzi wa wajumbe uahirishwe mpaka kikao kijacho.
(v) Matumizi ya sentensi kamili mf. Imeamuliwa kuwa mjadala uendelee katika kikao kijacho.
(vi) Matumizi makubwa ya vidokezo vya maana mf. Jambo la kwanza…vilevile…
(vii) Matumizi ya majedwali, vielelezo na michoro mbalimbali.

2. Mtindo wa kirasimi
Huu ni mtindo wa lugha rasmi ambao hupatikana katika mazungumzo na maandishi ya kwenye miktadha kama mahakamani, kwenye mikataba, barua rasmi, kumbukumbu, n.k

Sifa za mtindo wa kirasimi
(i) Matumizi ya mitindo mahususi
mf . - Ndugu mgeni rasmi
- Mheshimiwa hakimu (mahakamani)
- Ndugu, Yah:, wako mtiifu (barua rasmi)
(ii) Matumizi makubwa ya istilahi za kirasimu
mf. Idara, masijala, jalada, madai, n.k
(iii) Matumizi ya sentensi ndefu
mf. Endapo upande mmoja kati ya pande hizi zinazoingia mkataba utapenda kujitoa, upande unaojitoa utaulipa upande unaobakia kiasi cha shilingi milioni moja kama gharama za usumbufu.
(iv) Matumizi ya maneno yanayotaja vyeo
mf. – mwenyekiti
- Mwalimu wa taaluma
- Meneja mauzo, n.k

3. Mtindo wa magazetini
Magazeti ni chombo cha habari kinachotumia lugha ili kuwasiliana na jamii. Magazeti mengi hutolewa kwa lengo la kibiashara tofauti na machapisho mengine. Mara nyingi gazeti hutolewa kwa ajili ya siku moja tu na ikipita gazeti nalo huwa limepitwa na wakati isipokuwa kwa marejeleo maalumu.

Hali hiyo huathiri sana mtindo wa lugha kwani waandishi hupaswa kutumia lugha yenye ushawishi mkubwa kwa wateja na (wasomaji).

Sifa za mtindo wa Magazetini
(i) Huchanganya mitindo mbalimbali kwa sababu gazeti moja huwa na makala tofautitofauti.
(ii) Matumizi ya tamathali za usemi
Mf. – Timu ya riadha yaangukia ua
- Mnyama alishwa lambalamba chamazi
- Jangwani hoi kwa wakata miwa wa mtibwa
(iii) Matumizi ya misimu (simo)
mf. - Kibosile abambwa laivu akifanya yake na denti
- Mwalimu amkojoza mwanafunzi darasani
(iv) Matumizi ya wakati uliopo
mf. – Waziri akemea watendaji wabovu
- Uchaguzi kufanyika Oktoba
(v) Matumizi ya visawe vya maneno
Mf. – Mpira wa miguu, kabumbu, gozi, ndinga, soka
- Timu yafungwa, yabamizwa, yabugizwa, yatwangwa
(vi) Matumizi ya istilahi
Mf. – Mhariri, mwandishi wetu, maoni ya wasomaji, n.k
4. Mtindo wa mazungumzo yasiyo rasmi
Mazungumzo yasiyo rasmi ndiyo yanayochukua nafasi kubwa katika matumizi ya kila siku. Mazungumzo haya hufanywa bila ulazima wa kuzingatia kanuni za lugha.

Sifa za mtindo usio rasimi
(a) Mada huzuka papo hapo
(b) Mada zaidi ya moja huweza kuzungumzwa
© Matumizi makubwa ya misimu na tamathali za usemi
(d) Matumizi ya sentensi zisizokamili mf. Nilipotua pale nika…..si unajua…
(e) Matumizi ya vifupisho vya maneno mf. Anaishi DOM, ansoma UDSM.
(f) Matumizi makubwa ya tanakali sauti mf. Anajipitisha pale fya,fya,fya
- Alipiga yowe uuwiiii…..
REJESTA
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika.

AINA ZA REJESTA
1. Rejesta za Mitaani

Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke)n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka wa wazungumzaji wenyewe.

2. Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
- Maofisini au mahali popote pa kazi
- Mahakamani
- Hotelini
- Hospitalini
- Msikitini
- Kanisanin.k
(a) Mazungumzo ya hotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
A: Nani wali kuku?
B: Mimi
A: Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A- anapouliza “Nani wali kuku”: ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaye “wali kuku”.
(b) Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi: Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi: Sijui.
Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashitaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.
3. Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi, ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
- Vijana wenye rika moja,
- Wazee wenyewe,
- Wanawake wenyewe,
- Wanaume wenyewe,
- Mwalimu na mwanafunzi,
- Meneja na wafanyakazi wake,
- Mtu na mpenzi wake, n.k.
Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.

Mfano:
'Basi, Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana’
‘Basi nilizamia info kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga’
‘Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa noma kila mzamiaji’
Alikuwa mnoko kishenzi’
‘Akatema mkwara mbuzi, nikajibu kwa mkwara dume....akabloo mimi ndani’.
Maana ya Maneno
Wikiendi – Mwisho wa wiki.
Kibaridi –tulivu.
Kuzamia info – Kuingia mahali bila kualikwa.
Zinga la Mnuso –sherehe kubwa.
Saiti –sehemu.
Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni.
Noma – Hatari.
Mnoko kishenzi – kinaa sana
Mkwala mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.
4. Rejesta za Kitarafa
Hii ni lugha iliyozoeleka eneo Fulani na ikitoka nje ya mipaka yake huwa ni vigumu kueleweka.
mf.
- Kiswahili cha Kiyao
mf. Juma amenitona (amenifinya)
- Kiswahili cha Kingoni
mf. Mtambo mrefu (muda mrefu)
- Kiswahili cha Kimakonde
mf. Achante chana (asnate sana)


5. Rejesta Rasmi
Huu ni mtindo wa lugha ulioenea nchi nzima hata kuvuka mipaka ya nchi. Mara nyingi huwa ni lugha rasmi ambayo husanifishwa kwa mfano Kiswahili ni rejesta rasmi itumiwayo katika Nyanja zote za elimu, biashara, siasa na masuala ya kisayansi. Kiswahili kinatokana na lahaja ya Kiunguja.

DHIMA YA REJESTA
(a) Rejesta hutumika kutambulisha makundi mbalimbali ya watu kupitia mazungumzo yao wawapo popote.
(b) Rejesta hupunguza ukali na utusi wa maneno. Baadhi ya watu hutumia rejesta kama njia ya kuficha maneno makali.
© Rejesta hurahisisha mawasiliano na utoaji wa huduma maeneo yenye wahitaji wengi na wahudumu wachache.
(d) Rejesta hupamba lugha kutokana na mchezo wa maneno yanayotumiwa na wazungumzaji.
(e) Rejesta hukuza lugha kutokana na kusanifishwa kwa maneno maya yanayopata mashiko kupitia rejesta mf. Chakachua, uhujumu uchumi, n.k
Sababu za Kutokea kwa Rejesta
1. Ubinafsi
Baadhi ya watu hupenda kujitofautisha na watu wengine katika usemaji wao na matokeo yake ni kuibua mtindo wa lugha.
2. Mwingiliano
Mwingiliano wa watu ndani ya jamii huchochea pia kuibuka kwa mitindo ya usemaji miongoni mwa wanajamii husika.
3. Kupita kwa wakati
Mabadiliko ya kihistoria katika jamii huipa jamii msukumo wa mabadiliko ya matumizi ya lugha na kuibua mitindo mbalimbali ya uzungumzaji.
Mf. Kipindi cha Azimio la Arusha, uhujumu uchumi, siasa za vyama vingi hadi sasa kumeibuka maneno mbalimbali kuendana na kila wakati.
4. Shughuli zilizopo
Shughuli inayotawala eneo fulani pia huchochea kuibuka kwa mitindo mbalimbali ya lugha inayoendana na shughuli husika.
5. Matumizi ya uficho
Baadhi ya watu hasa vijana huibua mitindo mingi ya lugha ili kufanya mawasiliano yao yawe siri.
6. Tofauti za hadhi
Matabaka ndani ya jamii pia huchangia kuibuka kwa rejesta ambazo huelezea hadhi ya kundi husika dhidi ya makundi mengine.MISIMU (SIMO)
Misimu ni maneno yasiyo sanifu yanayozushwa na kikundi kidogo cha watu ili kuelezea utamaduni wa kikundi husika.

Misimu huweza kudumu na kupata mashiko hata kusanifishwa kuwa msamiati rasmi au kutoweka pale inapokosa mashiko.

CHANZO CHA MISIMU

(a) Mabadiliko ya kihistoria
Misimu huzuka kutokana na mabadiliko ya nyakati katika jamii, mabadiliko hayo huchochea kuibuka kwa maneno yasiyo sanifu ndani ya jamii.

(b) Hali ya utani
Baadhi ya misimu huzuka kutokana na watu kutaniana miongoni mwao na hata kuitana majina fulani fulani.

© Mwingiliano baina ya watu
Maingiliano baina ya watu wa jamii tofauti pia huchangia kuibuka kwa misimu mbalimbali.

(d) Kugunduliwa kwa dhanna mpya
Ugunduzi wa dhanna kama za kisayansi na kiteknolojia nako huibua misimu kutokana na dhanna hizo kupachikwa maana za kimisimu mf mashine za kiotomotela, kisimbuzi (king’amuzi), n.k
Sababu za Kutumia Misimu
(a) Kufanya mawasiliano yawe siri dhidi ya watu wasiohusika.
(b) Hali ya ujana kudhani matumizi ya misimu ndio kujuwa lugha vyema
© Kurahisisha mambo, baadhi ya watu hutumia misimu ili kurahisisha kueleweka kwao na kufanya wanayoyasema yaonekane mepesi.
(d) Kupunguza utusi na ukali wa maneno yasiyotamkika kirahisi

Njia za Kuunda Misimu
1. Kufupisha maneno
Mf. Ku - DISCO

2. Kutohoa toka lugha za kigeni
Mf. Fegi (fag), Antisosho (Antisocial)

3. Kutumia sitiari
Mf. – Amevaa chupa – (suruali nyembamba)
- Unga wa yanga – (unga wa njano)

4. Kutumia tanakali
Mf. Mataputapu, malapa


5. Kubadili maana ya msingi
Mf. – nyambizi
- Mikasi
- Kumfia mtu
Sifa za Misimu
(a) Kuzuka na kutoweka
(b) Huwa na chmvi nyingi
© Huwa na maana nyingi mf. Nimekumaindi
(d) Hupendwa sana hasa na vijana
(e) Huhifadhi historia ya jamii
Aina za Misimu
Misimu huweza kuwekwa kwenye makundi tofauti tofauti kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.
1. Kigezo cha mada
Kigezo hiki cha mada kinatupatia aina zifuatazo:
(i) MIsimu inayohusu pesa
- kuwaka/kuchacha/kukosa fedha
- kumtoa mtu upepo
- kuzunguka mbuyu
- kuchuna buzi, n.k

(ii) Misimu ya vyakula
Mf. – ubweche,cheka na watoto (wali)
- Bondo, nguna, (ugali)
- Pembejeo, magereza, (maharage)

(iii) Misimu ya ulevini
Mf. – juwa tungi/bwaksi
- Kukata maji
- Lete kama tulivyo

(iv) Misimu ya nguo
Mf. – kimodo
- Pensi nyanya
- Fundi tafadhali
- Kipedo
(v) Misimu ya usafiri
Mf. – vipanya
- Daladala
- Wa kusoma
- Kula kichwa
(vi) Misimu ya wanawake
Mf. – kishtobe
- Dogodogo
- Handiauti

2. Kigezo cha makundi ya watu
- Misimu ya wanafunzi
- Misimu ya wafanyabiashara
- Misimu ya magazetini

3. Kigezo cha jumla
(i) Misimu ya kawaida
Mf. – kujaa tele – kuwa na fedha
- Chai – hongo/rushwa
(ii) Misimu ya kujitokeza
Mf. – ganja – bangi
- Chauchau – rushwa
- Kidenishi – msichana
- Kidume – mvulana
Makundi yote hayo huweza kuwekwa katika aina kuu tatu za misimu ambazo ni:
1. Misimu ya pekee
Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.

2. Misimuya kitarafa
Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya, tarafa au mkoa.

Misimu hiimara nyingi hutokana na mambo kama vile:
- Vitu vilivyomo
- Lugha inayotumika
- Uzoefu wa mazingira


3. Misimu zagao
Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.

Mf:
- Wafurukutwa
- Wakereketwa
- Wapambe
- Ufisadi
- Ngangari
- Buzi
- Chakachua
- Kufulia
MATUMIZI YA MISIMU
1. kukuza lugha
Baadhi ya maneno yanayoibuka kama misimu husanifishwa na kuwa msamiati rasmi wa lugha na kuikuza lugha.

2. kupamba lugha
Matumizi ya misimu huifanya lugha iwe na mvuto miongoni mwa watumiaji wake

3. kurahisisha mawasiliano
Watumiaji wa misimu huelewana kirahisi na haraka zaidi kuliko wanapotumia lugha sanifu

4. Misimu hupunguza ukali na utusi wa maneno

5. Kuunganisha watu
Misimu hupunguza tofauti za watu kiumri na hata kiuchumi na kuwafanya waongee kwa namna moja.

6. Kuhifadhi historia ya jamii
Baadhi ya misimu hukumbatia historia ya jamii husika kwa kipindi kirefu cha jamii husika.

7. Kuibua hisia
Baadhi ya misimu hubeba hisia mbalimbali za wasemaji na kuelezea hisia hizo kupitia mazungumzo yao.


ATHARI ZA MISIMU

(a) Misimu huharibu lugha kwa sababu sio maneno sanifu
(b) Misimu hingiza msamiati wenye matusi katika lugha
© Hupunguza hadhira kwa sababu watu wengi huwa hawaelewi lugha ya mafumbo
(d) Misimu huwa na chumvi nyingi kwa hiyo haiaminiki
(e) Huzuka na kutoweka hivyo si ya kutegemewa
(f) Huwa na maana nyingi hivyo huleta kutoelewena.
UMAHIRI KATIKA LUGHA
Umahiri wa lugha ni ujuzi wa hali ya juu alionao mtu katika lugha kupitia stadi zote nne za lugha ambazo ni:
- Kuzungumza
- Kusikiliza
- Kusoma
- Kuandika
Umahiri wa lugha waweza kuhusu lugha moja au lugha zaidi ya lugha moja.
SABABU ZA UMAHIRI WA LUGHA
(a) Kusomea lugha kwa kiwango cha juu.
(b) Kuitumia lugha kwa muda mrefu na kila siku
© Kuepuka athari ya lugha nyingine hususan kikabila
(d) Kuwa karibu na wajuzi wa lugha kwa muda mrefu
(e) Kuwakosoa na kuwasahihisha watu wengine
ATHARI ZA UMAHIRI
1. Athari za kimatamshi
Baadhi ya watu hupata tabu ya kutamka baadhi ya sauti kutokana na athari ya lugha zao za asili.
Mf:
- Wakurya husema kurara badala ya kulala
- Wanyakyusa husema fyatu badala ya viatu
- Wapare husema thamaki badala ya samaki
- Wachaga husema subu badala ya supu
2. Athari za msamiati
Kumudu lugha zaidi ya moja huchochea uchanganyaji wa msamiati.
Mf:
- Kuwa standby badala ya kuwa tayari
- Nitakubeep badala ya nitakutonya
- Niliona missed call yako badala ya niliona simu fifi yako

3. Athari za kimuundo (Kisarufi)
Baadhi ya wazungumzaji huchanganya miundo ya lugha wanazozimudu kutokana na umahiri walionao.
Mf.
- Huyu mtoto ni mkorofi (Kiingereza)
- Mtoto huyu ni mkorofi (Kiswahili)

4. Athari za kimaana
Kumudu lugha zaidi ya moja kwa kiwango cha kawaida hufanya wazungumzaji waweze kung’amua maana angavu kwa kila msamiati hasa wanapobadili msimbo.
Mfano: Kinyamwezi neon “Igolo” lina maana ya “Jana” “Keshokutwa” kwa mantiki hii ni rahisi kumkuta mnyamwezi akisema.
- Nitakuja jana
- Nilikwenda kesho kutwa
LUGHA YA MAZUNGUMZO NA LUGHA YA MAANDISHI
1. Lugha ya mazungumzo
Huu ni utanzu wa mawasiliano unaomwezesha mtu kufikisha mawazo yake kwa njia ya mazungumzo yam domo. Lugha ya mazungumzo chanzo chake ni kuzungumza na kikomo ni kusikiliza.

MAMBO YA KUZINGATIWA NA MZUNGUMZAJI
 Kuzungumza kwa sauti ya kusikika
 Kutumia lugha kwa usanifu na ufasaha
 Mpangilio mzuri wa mawazo
 Uwazi na ukweli wa kinachozungumzwa

MAMBO YA KUZINGATIWA NA MSIKILIZAJI
 Utulivu na usikivu
 Kuelekeza mawazo katika kinachosikilizwa
 Kubaini wazo kuu
 Kuhusisha kinachosikilizwa na mazingira halisi.

2. Lugha ya maandishi
Ni utanzu wa mawasiliano unaomwezesha mtu kufikisha ujumbe au hisia zake kwa njia ya maandishi. Lugha ya maandishi chanzo chake ni kuandika na kikomo ni kusoma.
TOFAUTI YA LUGHA YA MAZUNGUMZO NA LUGHA YA MAANDISHI

(a) Uwasilishaji
Lugha ya mazungumzo huwasilishwa kwa njia ya mazungumzo na lugha ya maandishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.

(b) Chanzo na kikomo
Lugha ya mazungumzo chanzo ni kuzungumza na kikomo ni kusikiliza lakini lugha ya maandishi chanzo ni kuandika na kikomo ni kusoma.

© Uhusiano na hadhira
Lugha ya mazungumzo hukutanisha mzungumzaji na msikilizaji lakini lugha ya maandishi haimkutanishi mwandishi na msomaji.

(d) Mabadiliko
Lugha ya mazungumzo huweza kubadilika kulingana na wakati na mazingira lakini lugha ya maandishi haiwezi kupokea mabadiliko.

(e) Maandalizi
Lugha ya mazungumzo haina maandalizi lakini lugha ya maandishi inahitaji maandalizi.

(f) Uhifadhi
Lugha ya mazungumzo huhifadhiwa kichwani lakini lugha ya maandishi huhifadhiwa katika maandishi kwa kumbukumbu za baadaye.

(g) Wahusika
Lugha ya mazungumzo ina wahusika wengi lakini lugha ya maandishi ni kwa wale wanaojua kusoma na kuandika tu.

(h) Gharama
Lugha ya mazungumzo haina gharama ikilinganishwa na lugha ya maandishi.

(i) Matumizi ya sauti (Fonimu)
Lugha ya mazungumzo inatoa uhuru wa kimatamshi kama kiimbo, shadda, kidatu na toni tofauti na lugha ya maandishi.
MAKOSA KATIKA LUGHA
Lugha ndicho chombo muhimu cha mawasiliano baina ya watu wa jamii moja. Ili watu waweze kuitumia lugha kwa kuelewana, lazima pawepo utaratibu au sharia zinazotawala utumiaji wa lugha. Mzungumzaji akikiuka kanuni za lugha, anazungumza lugha potofu. Upotoshaji huu hujitokeza katika sarufi na kwenye mantiki. Makosa katika sehemu zote mbili husababisha kukatika kwa mawasiliano au kutoa ujumbe usiokusudiwa.


Mifano:
(a) Nimenunua chiti jana (Nimenunua kiti jana)
(b) Ukifika pale upige holi (Ukifika pale upige hodi)
© Jana nilivyoondoka hukuwepo (Jana nilipoondoka hukuwepo)

Sentensi (a) na (b) hukata mawasiliano, msikilizaji asijue maana inayokusudiwa. Hii ni kwa sababu, maneno “chiti” na “holi” hayafahamiki au hayatumiki kwa namna hiyo. Sentensi © inatoa maana isiyokusudiwa, msemaji anaelezea namna ya kuondoka badala ya wakati wa kuondoka.

Kwa hiyo lugha inapotumika vibaya huweza kupotosha lengo la msemaji. Makosa haya yanaweza kujitokeza katika sarufi na mantiki.

MAKOSA YA KISARUFI
Taratibu za lugha hutawala matamshi ya maneno, miundo ya tungo na maumbo ya maneno. Makosa ya kisarufi yanaweza kugawanywa katika sehemu zifuatazo:
(i) Makosa ya kimsamiati
Baadhi ya watu huchanganya msamiati wakati wa kuzungumza. Watu hutumia msamiati usiolingana na maana iliyokusudiwa.
Mfano:
- Watu huchanganya neon “nona” na “nenepa” wengi husema “siku hizi umenona sana.” Hii si sahihi kwani mtu husemwa “amenenepa” na mnyama husemwa kuwa amenona.
- Vilevile watu huchanganya neon “mazingira” na “mazingara.” Wengi husema, “mazingara yameharibiwa sana siku hizi.” Hii sio sahihi na sahihi ni kusema “Mazingira yameharibiwa sana siku hizi”
- Maneno mengine ni “ajali” na “ajili.” Watu husikika wakisema “Asha alifariki kwa ajili ya gari moshi” badala ya kusema “Asha alifariki kwa ajali ya gari moshi”
- Maneno engine ni “wakilisha” na “wasilisha.” Watu husema, “waziri wa fedha atawakilisha bajeti ya mwaka huu bungeni” badala ya kusema “waziri wa fedha atawasilisha bajeti ya mwaka huu bungeni.”
Makosa ya kimsamiati yanatokana na mazungumzaji kutokuwa na ujuzi wa kutosha wa msamiati wa lugha anayoitumia au wakati Fulani yanatokana na utani miongoni mwa wazungumzaji. Kwa mfano matumizi ya “nona” kwa kumuelezea mtu mnene yanatokana na kuambiana hivyo kwa utani lakini hatimaye watu wakalichukua neon hilo katika matumizi ya kawaida.

(ii) Makosa ya kimuundo
Makosa mengine yanayojitokeza ni katika muundo. Sentensi za Kiswahili kwa kawaida huanza na nomino ya mtenda au mtendwa na huwa na vitenzi.
Mfano:

(a) Huyu mtoto ni mkorofi
x N t V

Sahihi inapaswa kuwa:

(b) Mtoto huyu ni mkorofi
N V t V

Sentensi (a) imetumia muundo wa lugha ya Kiingereza na sentensi (b) imezingatia muundo wa Kiswahili.

Katika makosa ya kimuundo, vilevile kuna tatizo la upatanisho wa kisarufi. Watu hupotosha au kuchanganya upatanisho wa kisarufi.

Mfano:
- Watu husikika wakisema, “sikuwa ninajua kuwa Tunu ni dada yako” sahihi ni kuwa, “Sikujua kuwa Tunu ni dada yako”
- Wengine husema, “Sisi wote tunapenda nyama” badala ya kusema; “Sisi sote tunapenda nyama”
- Pia kuna wanaosema, “Nimekuja hapa ili kusudi niongee na nyinyi.”Hili ni kosa kwa sababu neon “ili” na “kusudi” hayawezi kufanya kazi ppamoja, sahihi ingekuwa “nimekuja hapa ili niongee na nyinyi au nimekuja hapa kusudi niongee na nyinyi”.

(iii) Makosa ya kimatamshi
Wakati mwingine makosa hujitokeza katika matamshi. Watu wengi hushindwa kutamka baadhi ya sauti za Kiswahili au wakati mwingine huchanganya na kubadili sauti hizo.

Mfano:
- Wakurya hutumia r badala ya l
Mimi naenda kurara – mimi naenda kulala
- Wandali (ileje) hutumia s badala ya z, dh na th.
Selasini – thelathini
Sahabu – dhahabu
Samani - dhahabu
- Wapare hutumia th badala ya s
Thamaki - samaki
- Wanyakyusa hutumia f badala ya vy
Fiatu fyangu – viatu vyangu

Kwa kawaida makosa ya kimatamshi yanatokana na athari ya lugha mama (lugha ya kwanza). Kwa kuwa Kiswahili ni lugha ya pili kwa wazungumzaji wengi, hivyo lugha ya kwanza inakuwa na athari kubwa kwa mtu anayejifunza lugha ya pili.

(iv) Makosa ya kuongeza vitamkwa/viambishi
Baadhi ya wazungumzaji huongeza vitamkwa mahali pasipohitajika na hivyo kuharibu lugha.

Mfano:
- Amekwendaga kwao – badala ya amekwenda kwao.
- Mtoto msafi – badala ya mtoto safi
- Msichana mhodari – badala ya msichana hodari
- Vitabu vipo mashuleni – badala ya vitabu vipo shuleni
- Bwana yule huwaga hapendagi fujo – badala ya bwana yule huwa hapendi fujo.

Kwa kwaida makosa ya kuongeza vitamkwa/viambishi yanatokana na athari ya lugha mama (lugha ya kwanza), hasa athari ya Kisukuma au Kinyamwezi katika matumizi ya Kiswahili. Wasukuma na Wanyamwezi huongeza kitamkwa/kiambishi mwanzoni au mwishoni mwa neon wanapozungumza Kiswahili, ijapokuwa kosa hilo hufanywa hata na watu ambao lugha hizo si lugha zao za kwanza.

(v) Makosa ya kuacha maneno
Wazungumzaji wengine huacha maneno fulani katika sentensi na bado wakafikiri wanatoa ujumbe uleule wa awali.

Mfano:
- Damasi ameondoka kazini – mzungumzaji anakusudia kusema “Damasi ameondoka kuelekea kazini” lakini anatoa ujumbe kuwa “Damasi ameondoka (hayupo tena) kazini.” Sentensi hii inatoa maana ambayo ni kinyume kabisa na ile inayokusudiwa na mzungumzaji.
- Wewe mtoto baba yako amerudi kutoka kazini? mzungumzaji hapa anakusudia kuuliza kama “Baba amerudi kutoka kazini.” Kwa kuliacha neno “kutoka” mzungumzaji anatoa maana ambayo ni kinyume kabisa na ile maana aliyokusudia. Swali lake linataka kujua kama – “Baba amekwenda tena (amerudi) kazini,” n.k

(vi) Makosa ya tafsiri sisisi
Hii ni tafsiri ya neon kwa neon. Tafsiri ya neon kwa neon nayo inaleta matatizo ya kisarufi katika lugha.

Mfano:
- Oshwa na mvua
“Katika mafuriko ya juzi nyumba mbili zimeoshwa na mvua”. Sentensi hii ina makosa. Sentensi sahihi ingekuwa: “Katika mafuriko ya juzi nyumba mbili zimechukuliwa na maji ya mvua.”
Sababu ya kosa hili ni tafsiri ya moja kwa moja kutoka lugha ya Kiingereza “wash out”. Athari ya kufikiri kwa Kiingereza na uwezo mdogo wa kutafsiri maneno hayo kwa Kiswahili.
- Kosa linguine liko katika matumizi ya maneno Aidha………au. Wakati huu aidha yuko mjini au kazini”. Hapa kuna kosa, sahihi ingekuwa hivi “Wakati huu yuko mjini aidha kazini………au iwe……wakati huu yuko mjini au kazini”.
Sababu ya kosa hili ni tafsiri sisisi kutoka Kiingereza ya either….or…muundo ambao hauko katika Kiswahili. Katika Kiswahili neon “aidha” lina maana ya “isitoshe”, “zaidi ya hayo”, n.k. Na mara nyingi huwa mwanzoni mwa sentensi.
- Kosa linguine ni matumizi ya neon osha uso. “Kwa kuwa ni asubuhi sina budi kuosha uso.” Sentensi hii ina makosa, sentensi sahihi ni “Nawa uso”. “Kwa kuwa ni asubuhi sina budi kunawa uso”. Sababu ya kosa hili ni tafsiri sisisi kutoka Kiingereza ya “Wash my face.”

Kwa ujumla makosa ya kisarufi ni mengi na yanategemea sana mazingira Fulani hutokea zaidi kwenye jamii za watu wa maeneo fulani.

MAKOSA YA KIMANTIKI
Mantiki ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Makosa ya kimantiki ni yale yanayoonesha kukosekana kwa utaratibu wa kifikra. Ni makosa yanayotokana na upotofu wa mawazo ya mzungumzaji.

Mfano:
Watu wengi husikika wakisema hivi:
- Usimwage kuku kwenye mchele mwingi. badala ya kusema usimwage mchele kwenye kuku wengi.
- Nyumba imeingia nyoka badala ya kusema Nyoka ameingia ndani ya nyumba.
- Chai imeingia inzi – Kwa kawaida inzi ndiye anayeingia kwenye kikombe cha chai. Chai haina uwezo wa kumwingia inzi. inzi ameingia kwenye chai.
- Rashidi amejenga hoteli mpya tena inakula watu – Kwa kawaida watu ndio wanaokula vyakula kwenye hoteli. Hoteli haili watu. Rashidi amejenga hoteli na inapata wateja wengi.
Kusahihisha Makosa
Katika lugha yoyote ile, makosa ya kawaida yataendelea kuwepo. Jambo lililopo ni kujaribu kuyazuia kabisa yasitumike katika taasisi rasmi kama vile shuleni, vyuoni, kwenye barua na mikutano ya kikazi, vyombo vya habari, sehemu za hadhara, n.k
Kuhusu makosa ya kisarufi kwa ujumla, jitihada za marekebisho sharti zitiliwe maanani tangu kiwango cha elimu ya msingi. Tafsiri za lugha ya kwanza zinazoathiri Kiswahili zikifanywa, bila shaka zitasaidia sana katika kuwapa waalimu mwanga kuhusu makosa yanayohitaji masahihisho.
Makosa ya msamiati husambazwa zaidi na vyombo vya habari na wakati mwingine hata na walimu. Pengine ingekuwa jambo zuri kama somo la matumizi ya Kiswahili lingesisitizwa katika vyuo vyetu vya ualimu.
UTATA WA TUNGO
Tungo tata ni ile yenye maana zaidi ya moja, na aghalabu maana zenyewe haziko wazi kabisa. Sentensi moja inaweza kueleweka hivi au vile, na kila maana ikawa sahihi katika mazingira yake.
Mfano:
(i) Mtoto anaendesha – utungo huu unaweza kutoa maana kuwa:
• Mtoto ana uwezo wa kuendesha chombo cha barabarani,angani au baharini.
• Mtoto ana maradhi ya tumbo la kuhara.
(ii) Juma amenunua mbuzi – utungo huu unaweza kueleweka kuwa:
• Juma amenunua chombo cha kukunia nazi
• Juma amenunua mbuzi mnyama afugwaye
(iii) Nyumba imebomolewa nini?
• Mtu ametumia (chombo) nini kubolea nyumba?
• Mtu amekuwa na sababu ipi iliyomfanya aibomoe nyumba?
• Nyumba imebomolewa sehemu gani?
(iv) Shuleni kwetu hatuna mwalimu wa Kiingereza
• Shuleni kwetu hatuna mwalimu anayefundishwa Kiingereza
• Shuleni kwetu hatuna mwalimu mwenye uraia wa Uingereza
Sababu za utata
(i) Neno kuwa na maana zaidi ya moja “endesha” na “mbuzi” katika sentensi ya kwanza nay a pili hapo juu.
(ii) Kutozingatia kanuni za uandishi.
Mfano I
(a) Tulimkuta Juma na rafiki yake, Meshaki
(b) Tulimkuta Juma na rafiki yake Meshaki
Sentensi (a) ina maana kuwa tuliwakuta watu wawili yaani Juma na rafiki wa Juma. Rafiki huyo anaitwa Meshaki: Alama ya mkato baada ya neon “yake” huonesha kuwa taarifa imekamilika na neon “Meshaki” ni ufafanuzi tu wa “Rafiki yake”.
Sentensi ya (b) ina maana kwamba tulimkuta Juma na mtu mwingine ambaye ni rafiki wa Meshaki.
Mfano II
Baba John amefika
Sentensi hii inaweza kutenganishwa na kutiwa mkazo sehemu mbalimbali kama ifuatavyo:
- Baba, John amefika
- Baba John, amefika
- Baba John amefika
(iii) Kutumia maneno bila kuzingatia mazingira au muktadha unaohusika na matumizi ya maneno hayo.
Mfano:
Mwajuma ametumwa na Rama
Katika sentensi hii, msikilizaji na mzungumzaji wataelewana iwapo wote wanawajua Mwajuma na Rama na hali ya uwezekano wa yupi wa kumtuma nani.
(iv) Utumiaji wa maneno yenye maana / lugha ya picha iliyofichika, yaani viashiria.
Mfano:
Nina ua nyumbani pangu
• Nina wigo
• Sehemu yam mea
• Natoa watu maisha
• Binti mzuri (Lugha ya picha)
(v) Matumizi ya vitenzi vyenye kauli ya kutenda au kutendewa
Mfano:
Peter ameuawa na simba
- Simba amemuua Peter
- Peter amemuua simba
- Simba na Peter wameuawa na mtu fulani.
(vi) Kuwepo kwa mofu ya kauli ya kutendea
Mfano:
Juma alimpigia ngoma Asha
- Juma alimpiga Asha kwa sababu ya ngoma
- Juma alipiga ngoma kwa niaba ya Asha
- Juma alipiga ngoma ili kumfurahisha na kumburudisha Asha.
(vii) Kuwepo kwa kiambishi nafsi kiambata A-Wa
Mfano:
• Alisema atakutembelea.
- Mtu huyo atakutembelea wewe
- Mhusika huyo anakuambia mtu mwingine atakutembelea
• Baba atawatuma sokoni
- Baba atawatuma nyinyi sokoni
- Baba atawatuma wahusika wengine sokoni
(viii) Matumizi ya baadhi ya viunganishi
Mfano
• Nilikuwa na Juma na watoto wake.
- Juma aliambatana na watoto wake
- Nilikutana na Juma, kasha nikakutana na watoto wa mtu mwingine.
(ix) Matumizi ya baadhi ya vihusishi
Mfano:
• Juma hapendi kusoma kama Damasi
- Wote hawapendi kusoma
- Juma hapendi kusoma ila Damasi amezidi
(x) Matumizi ya vimilikishi
Mfano:
• Frenki atajenga kibanda chake
- Frenki atajenga kibanda atakachokimiliki yeye
- Frenki atajenga kibanda cha mtu mwingine
• Mercy alisema atakwenda kwao
- Mtu fulani atakwenda kwa akina Mercy
- Mercy atakwenda kwa mhusika fulani
- Mercy atakwenda anakoishi na wazazi wake
(xi) Matumizi ya mzizi “ingine”
Mfano:
• Kingine kimepatikana
- Kitu kingine zaidi ya hiki kimepatikana
- Kingine kimepatikana badala ya hiki
• Wengine hawahitajiki
- Wengine zaidi ya hawa hawahitajiki
- Wengine baadhi ya hawa hawahitajiki
- Wengine badala ya hawa hawahitajiki
Kuondoa Utata
 Katika lugha ya mazungumzo kuwe na mkazo tofauti wa sauti kuonesha kwamba neno lipi lipewe uzito zaidi
 Kuzingatia matumizi sahihi ya alama za uandishi katika maandishi
 Matumizi sahihi yenye kuleta utata
 Kuepuka makosa ya kisarufi na kimantiki yasiyo ya lazima
 Uteuzi mzuri wa maneno hasa yenye kubeba maana zaidi ya moja
 Kuwa makini na matumizi ya maneno yenye maana ya picha.
MATUMIZI YA KAMUSI
Kamusi ni kitabu cha marejeleo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani, na kupangwa kwa utaratibu maalumu, kasha kufafanuliwa kwa namna ambayo msomaji huweza kuelewa.
Ufafanuzi wa msamiati unaoingizwa kwenye kamusi ni fasili na maelezo mengine kulingana na lengo la kamusi husika.
Msamiati unaoingizwa katika kamusi waweza kuwekwa katika makundi makuu mawili: (a) maneno yote ya lugha au fani fulani (b) orodha ya maneno yaliyochaguliwa kutoka katika lugha ya kawaida au lugha ya fani fulani na kupewa maelezo mafupi ya maana za maneno hayo.
Mtunga kamusi huteua msamiati fulani anapotunga kamusi na kuacha mwingine. Uteuzi wa maneno yanayoingizwa katika kamusi huongozwa na vigezo vifuatavyo:
(i) Umbo la neno
(ii) Maana ya neno
(iii) Historia ya neno
(iv) Matumizi ya neno
Kwa nini kamusi ilitungwa?
Utungaji wa kamusi ulianza katika jamii zilizojua kusoma na kuandika. Kamusi ilihitajika ili imsaidie mtumiaji kufahamu maana za maneno aliyoyasoma. Maneno haya yalipatikana katika matini mbalimbali kama vile vitabu na magazeti. Kwa sababu hii ni wazi kuwa, kamusi zilianza kutungwa ili kukidhi haja ya kupata maana ambazo hazikujulikana.
Jamii isiyojua kusoma na kuandika, hususani ile ambayo haikuingiliana na watu wa jamii nyingine yenye utamaduni tofauti haikuhitaji kamusi, hii ni kwa sababu kila mwanajamii alifahamu msamiati wote uliohitajika kwa mawasiliano.
Kwa hali hii ni dhahiri haja ya kamusi ilichochewa na kuongezeka kwa msamiati kutokana na kupanuka kwa matumizi ya lugha. Matumizi ya lugha yalipanuka ili kutosheleza haja ya kueleza na kufafanua dhanna mpya zilizotokana na kukua na kubuniwa kwa maarifa mapya yaliyojidhihirisha katika Nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia.
Muundo wa Kamusi
Kamusi imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: Utangulizi, matini ya kamusi na Sherehe ya kamusi.


1. Utangulizi wa kamusi
Hii ni sehemu ya mwanzo ya kamusi ambayo hutangulia matini yenyewe ya kamusi. Utangulizi hujumuisha muhtasari wa sarufi ya lugha yenyewe pamoja na maelezo ya namna ya kuitumia kamusi. Utangulizi huonesha pia vifupisho vilivyotumika ndani ya kamusi na maana zake.
2. Matini ya kamusi
hii ni sehemu yenye vidahizo vyote vya kamusi husika kuanzia herufi ya alfabeti “A” hadi “Z”. Vidahizo vyote huorodheshwa hapa na kufafanuliwa. Taarifa mbalimbali za kiisimu huingizwa hapa. Taarifa hizo huhusu aina ya neno, maana (fasili) ya neno, vifupisho vya maneno, matumizi ya alama na vituo mbalimbali, matamshi, matumizi ya misemo, nahau, methali, n.k.
• Kidahizo ni neno lolote linaloingizwa kwenye kamusi na kutolewa fasili yake.
3. Sherehe ya kamusi
Sehemu hii ya Kamusi huingiza baadhi ya taarifa za ziada zenye msaada kwa mtumiaji wa kamusi. Taarifa zinazoingizwa sehemu hii ni kama vile:
• Majina ya nchi mbalimbali
• Vyeo vya kijeshi
• Vipimo mbalimbali vya urefu, ujazo, ukubwa, n.k.
Mpangilio wa maneno katika kamusi
Maneno yanayoingizwa katika kamusi nyingi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi A, yote huwekwa chini ya herufi A. Vivyo hivyo kwa maneno yanayoanza na herufi b, ch, d hadi z. maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano unavyoonesha hapa chini:
Mfano: jabali, jabiri, jadhibika, jadi.
Maneno yote yanaanza na herufi [j]. Herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. Herufi ya tatu ni . Kwa kuwa hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti, maneno yenye huorodheshwa kwanza kabla yay ale yenye [d]. Kwa vile maneno yenye ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya maneno hayo ili kuchagua neno litakaloorodheshwa mwanzo. Neno jabali litaorodheshwa kabla ya jabiri kwa kuwa [a] (herufi ya nne kwenye jabali hutangulia ya jabiri ambayo pia ni herufi ya nne. Kasha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya jadhibika na jadi. Kwa kuwa [h] hutangulia basi jadhibika litaorodheshwa mwanzo na kufuatiwa na jadi.
Taarifa za Kikamusi
Kamusi za siku hizi huwa na taarifa zaidi ya maana. Miongozi mwa taarifa ambazo kamusi huwa nazo ni:
1. Kidahizo
Kidahizo ni neno linaloorodheshwa katika kamusi ili litolewe maana zake pamoja na taarifa nyinginezo. Katika kamusi, vidahizo vinaorodheshwa ki- alfabeti na huandikwa katika chapa iliyokolezwa wino.
Mfano
Ardhi nm 1. nchi kavu udongo
2. dunia
Fuska nm: tabia mbaya, hasa ya uasherati.
2. Vibadala
Kibadala ni kimoja kati ya maneno au zaidi yanayotofautiana kidogo kimaandishi na kimatamshi lakini yenye maana sawa. Maumbo au matamshi hayo tofauti hutumiwa na watu wa maeneo tofauti au wa lahaja tofauti za Kiswahili. Kwa mfano, neno benki hutumiwa zaidi Tanzania na banki hutumiwa zaidi Kenya. Kama vibadala viwili vitabainika vyote ni sanifu au vina matumizi mapana, maumbo yote mawili yanaingizwa katika kamusi kama vile “alimradi na ilimradi” nm, aminifu – Amini, amwali – amuali, amin – amini, n.k.


3. Misemo (ms), methali (mt) na nahau (nh)
Taarifa nyingine zinazoingizwa katika kamusi ni misemo, methali na nahau. Taarifa hizi zinawekwa baada ya fasihi au mifano ya matumizi katika chapa ya italiki. Semi hizi hutengwa na taarifa zilizotangulia kwa nukta mkato (Wink na kutanguliwa na alama (ms) kwa misemo, (mt) kwa methali na (nh) kwa nahau.
Mfano
Adimika kt [sie]: patikana kwa uchache au kwa nadra; ghibu; (ms) ume – kama wali wa daku.
4. Kitomeo
Kitomeo ni neno linaloingizwa katika kamusi kama kidahizo pamoja na taarifa zake zote kama vile kategoria, idadi, sinonimu, n.k.
5. Michoro
Kamusi huingiza michoro ya vitu mbalimbali. Lengo la michoro hiyo ni kusaidia fasili kuelezea maana ambazo hazieleweki kwa urahisi.
6. Orodha ya nchi na utaifa
Taarifa nyingine zinazoingizwa katika kamusi ni orodha ya nchi na utaifa. Lengo la orodha hiyo ni kuwasaidia wazungumzaji na watumiaji wa lugha kuwa na namna moja ya kutaja majina ya nchi na utaifa. Orodha hii inawekwa mwishoni kabisa mwa kamusi.
7. Tahajia ya neno
Tahajia ni uwasilishaji wa sauti kwa herufi katika maandishi kufuatana na mwendelezo wa maneno uliokubaliwa. Maneno katika kamusi yanaandikwa kufuatana na tahajia sanifu. Kwa yale maneno yenye tahajia zaidi ya moja, basi lahaja zote zinaoneshwa.
8. Matamshi ya Maneno
Kamusi huonesha namna ya kutamka maneno yanayoingizwa katika kamusi ili kumwelekeza mtumiaji wa kamusi jinsi yanavyotamkwa. Matamshi ya maneno huoneshwa kwa kutumia alama za kifonolojia ambazo huonesha herufi zinazounda neno.
Maneno ya Kiswahili yanaandikwa kama yanavyotamkwa kwa hiyo hayahitaji alama za kuonesha namna ya kuyatamka. Isitoshe haja ya kuwa na maelekezo ya matamshi ya maneno ni muhimu kwa wanafunzi wa Kiswahili, hususan wageni ambao hawakuzoea sauti fulani ambazo hazipo katika lugha zao. Kwa mfano, Kiingereza hakina sauti inayowakilishwa na umbo /ng/ kama inavyodhihirika katika neno /ngoma/ japokuwa wanalo umbo kama hilo ambalo hutamkwa kama /ng’/ ya neno /ng’ombe/ na /th/ za Kiswahili huwakilishwa na umbo moja tu katika Kiingereza.
Kwa hali hii ni dhahiri kuwa, maelezo ya namna ya kutamka maneno ya Kiswahili siyo muhimu kwa kamusi iliyolenga wenyeji wa Kiswahili kama ilivyo Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Kamusi inayotungwa mahususi kwa wageni haina budi kuonesha namna ya kutamka kwa usahihi yale maneno ambayo ni magumu kutamka. Maneno yasiyokuwa na shida kutamka ambayo kwa hakika ni mengi katika Kiswahili yasiyooneshwa, kwani itakuwa kujaza nafasi bure.
9. Sarufi ya lugha
Sarufi ya lugha kama inavyojitokeza katika kila neno kama vile maumbo ya wingi wa nomino, vinyambuo vya maneno kama vile lima, limia, limika, limisha, limwa, n.k. ambayo hutokana na kitenzi “Lima”
10. Maana za maneno
Kamusi huonesha maana za maneno. Maana hizi zinaelezwa kwa kutoa fasili (maelezo) pamoja na maneno mengine yenye maana sawa au zinazokaribiana, yaani sinonimu. Kimpangilio, fasili hutangulia na sinonimu hufuata.
Kidahizo chenye maana zaidi ya moja huoneshwa maana zake kuu kwa kutumia tarakimu 1,2,3, n.k. Pale ambapo maana kuu ina maana nyingine ndogondogo, maana hizo zinaoneshwa kwa kuwekewa alama (a), (b), ©, (d), n.k. au tarakimu.


Mfano
Fungo1 nm (ma) (a) muda wa kujinyima kwa hiyari chakula, maji na vinginevyo; muda wa kufunga. (b) namna ya kufunga © dhamana
Fungo2 nm dawa inayotengenezwa kwa mizizi ya ndago ambayo husaidia meno ya mtoto kuota yakiwa imara.
Fungo3 nm mnyama kama paka mwitu na mdogo kuliko ngawa.
11. Etimolojia ya neno
Kamusi huonesha etimolojia ya neno, yaani asili ya neno, mfano neno fulani asili yake ni kutoka nchi gani au lahaja gani.
12. Matumizi ya maneno
Kamusi huonesha matumizi mbalimbali ya maneno. Kwa kawaida, maneno mengi ya lugha hutumiwa katika nyanja mbalimbali. Hata hivyo, kuna baadhi ya maneno hutumika zaidi katika maeneo fulani maalumu, kama vile dini, fizikia, baiyolojia, ushairi au sarufi. Maneno kama haya hupewa alama maalumu kuonesha maneno yanamotumika zaidi.
Mfano:
Kwaresima nm (kd) siku arubaini za mfungo wa wakristo kabla ya sikukuu ya pasaka.
Yambiwa nm (sarufi) kipashio cha sentensi kinachodokeza mtendewa.
AINA ZA KAMUSI
Kwa kutumia kigezo cha dhima au lengo la kamusi kuna aina zifuatazo za kamusi:
1. Kamusi wahidiya
Hii ni kamusi inayoandikwa katika lugha moja tu, na inalengwa kwa wazungumzaji wazawa wa lugha hiyo. Wakati mwingine huwafaa wanaojifunza lugha hiyo kama lugha ya pili au ya kigeni. Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, vidahizo vya kamusi wahidiya na maelezo ya maana ya vidahizo hivyo huwa katika lugha moja. Mfano wa kamusi wahidiya ni Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI iliyochapishwa mwaka 1981 na ile ya Oxford Advanced Learners Dictionary.
2. Kamusi thaniya
Hii ni kamusi iliyoandikwa kwa lugha mbili. Vidahizo huandikwa katika lugha moja (lugha chanzi) na maelezo ya maana ambayo aghalabu huwa neno moja, yaani visawe, huandikwa katika lugha ingine (lugha lengwa). Lengo la kamusi thaniya ni kumsaidia mtu anayefahamu lugha moja kati ya zilizotumiwa kujifunza lugha ingine, kuelewa matini anazosoma ambazo zimeandikwa katika lugha ya vidahizo vya kamusi na kumsaidia kujieleza vizuri hasa anapoandika katika lugha lengwa. Mifano ya kamusi thaniya ni kamusi za TUKI za mwaka 1996: Englisha – Swahili Dictionary, Kamusi ya Kiswahili – Kiingereza, Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) na Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia
3. Kamusi mahuluti
Hii ni kamusi yenye lugha zaidi ya mbili. Ni kamusi iliyoandikwa kwa lugha nyingi. Vidahizo vya kamusi mahuluti hupatiwa visawe katika lugha mbili au zaidi.
Mfano
Kiswahili Kiingereza Kijerumani
nyumba nm house haus
mtoto nm child kind
kitabu nm book buch
tembea kt walk laufen
4. Kamusi za kitaaluma
Hizi ni kamusi zinazoandikwa na wasomi ili zitumike katika uwanja fulani wa kitaaluma kama vile fizikia, kemia, biolojia, isimu, fasihi, n.k. Kamusi za aina hii huwa na maneno ya kitaaluma. Mfano wa kamusi za kitaaluma ni Kamusi Awali ya Sayansi na Teknolojia (1995), Kamusi ya Isimu na Lugha (1996), Kamusi ya Biolojia, Fizikia na Kemia (1996) Dictionary of Archaeology (1972).
5. Kamusi za semi
Kamusi za aina hii huwa na mkusanyiko wa semi kama vile nahau, methali, misemo, n.k. Kamusi hizi hueleza maana za semi mbalimbali na matumizi yake. Mfano wa kamusi za semi ni Kamusi ya Misemo na Nahau (2000) na Kamusi ya Methali (2001)
6. Kamusi za watoto
Hizi ni kamusi wanazotungiwa watoto, hasa katika madarasa ya chini. Sifa kubwa ya kamusi hizi ni wepesi wa maelezo na matumizi mengi ya picha. Mfano wa kamusi za watoto ni Kamusi ya Kwanza ya Kiswahili - Kiingereza
7. Kamusi za visawe
Hizi ni kamusi zenye kueleza maana za maneno kwa kutumia visawe vyake. Katika kamusi ya aina hii, neno kama vile ghilba huelezwa kwa visawe vyake kama vile uongo, ulaghai, hadaa, n.k.
Dhima ya kamusi
Kamusi ina umuhimu kwa mtumiaji yeyote wa lugha kwa sababu zifuatazo:
(a) Kamusi huonesha tahajia (spellings) sahihi za maneno
(b) Kamusi hueleza maana (fasili) mbalimbali za maneno
© Kamusi huonesha matamshi sahihi ya maneno
(d) Kamusi hubainisha aina (kategoria) ya neno
(e) Kamusi huonesha misemo, semi, misimu na methali mbalimbali
(f) Kamusi huonesha asili ya neno
(g) Kamusi huonesha alama na vifupisho mbalimbali vya lugha
(h) Kamusi huongeza maarifa zaidi kuhusu lugha ya mzungumzaji
(i) Kamusi husaidia kujifunza lugha za kigeni.
(This post was last modified: 06-18-2017 01:02 PM by MwlMaeda.)
06-18-2017 12:59 PM
Visit this user's website Find all posts by this user Like Post Quote this message in a reply
francissmtambo Offline
Regular User
Registered

Posts: 5
Likes Given: 3
Likes Received: 1 in 1 posts
Joined: Jun 2016
Reputation: 0
Friend:  Add as Friend

Points: 1.00 points
Post: #2
RE: Utumizi Wa Lugha

0
0
Samahani mofimu. Isimu. Kishazi. Hizi ni Aina gani ya lugha

Sent from my Phantom6-Plus using MyElimu mobile app
06-19-2017 08:16 PM
Find all posts by this user Like Post Quote this message in a reply
MwlMaeda Offline
Teacher
Teacher

Posts: 41
Likes Given: 1
Likes Received: 3 in 3 posts
Joined: Feb 2017
Reputation: 0
Friend:  Add as Friend

Points: 3,446.38 points
Country: Tanzania
Post: #3
RE: Utumizi Wa Lugha

0
0
Mofimu ni moja wapo ya vipashio vya lugha. Vipashio vingine ni neno, kirai,kishazi na sentensi.

Isimu ni sayansi ya lugha
06-20-2017 12:58 PM
Visit this user's website Find all posts by this user Like Post Quote this message in a reply
Post Reply 


You may also like these discussions:
Thread: Author Replies: Views: Last Post
  Matumizi Ya Lugha Katika Miktadha Mablimbali MyElimu 0 932 12-04-2017 02:24 PM
Last Post: MyElimu
  Umuhimu Wa Lugha Ya Kiswahili Sunday 0 2,604 09-21-2017 12:32 PM
Last Post: Sunday
Post Icon Lugha Kama Chombo Cha Mawasiliano MyElimu 0 2,473 09-14-2017 01:08 PM
Last Post: MyElimu
Post Icon Tabia Na Sifa Za Lugha MwlMaeda 0 474 06-07-2017 01:58 PM
Last Post: MwlMaeda
Post Icon Matumizi Ya Lugha Katika Miktadha Mbalimbali. Damian 3 1,577 05-23-2017 02:16 PM
Last Post: kemmyqlyon
Post Icon Nadharia Ya Ukuaji Na Ueneaji Wa Lugha MyElimu 0 5,710 02-07-2015 05:09 AM
Last Post: MyElimuUser(s) browsing this thread: 1 Guest(s)