Utungaji/uandishi
How to register and join MyElimu CLICK HERE

Post Reply 
 
Thread Rating:
  • 0 Votes - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
Utungaji/uandishi
MwlMaeda Offline
Teacher
Teacher

Posts: 41
Likes Given: 1
Likes Received: 3 in 3 posts
Joined: Feb 2017
Reputation: 0
Friend:  Add as Friend

Points: 3,446.38 points
Country: Tanzania
Post: #1
Utungaji/uandishi

0
0
UTUNGAJI/UANDISHI
Utungaji ni neno linalotokana na kitenzi “tunga”. Kitenzi hiki kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004:414) linamaanisha “toa mawazo kutoka ubongoni na kuyakusanya, kisha kuyadhihirisha kwa maandishi, kwa kusimulia, kwa kuyaimba au kwa muziki.
Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa, utungaji ni kutoa mawazo binafsi kutoka akilini mwa mtu kuhusiana na mambo mbalimbali katika jamii, kisha kuyaweka wazi kwa njia ya mdomo au maandishi.Kile kilichotungwa na mtunzi kinaweza kudhihirishwa kwa mitindo mbalimbali, kama vile riwaya, mashairi, tamthiliya, insha na barua.
Dhima ya Utungaji
· Utungaji huwezesha watu kutoa maelezo, mawazo au maoni kwa njia ya maandishi au mazungumzo.
· Utungaji huwezesha utumiaji wa lugha fasaha, sanifu na uwezo wa kujieleza kwa njia ya maandishi au mazungumzo.
· Utungaji huwezesha utumiaji wa mantiki, mpangilio mzuri wa mawazo, mtiririko na matumizi sahihi na fasaha ya lugha na kanuni za fasihi.
· Utungaji huwezesha kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu maisha yetu ya kila siku. Kupitia njia ya utungaji, watu hupata taarifa kuhusu vitu mbalimbali vinavyozunguka maisha yao ya kila siku.
· Utungaji hutumika kuelimisha, kukosoa na hata kuonya. Maandishi au mazungumzo (masimulizi) yanayotokana na utungaji huweza kuakisi hali halisi ya maisha ya jamii, na hivyo ikawa ni kama kioo cha kujitazama na kujirekebisha.
· Utungaji, hususan unaotokana na kazi za fasihi hutumika kuburudisha jamii. Hadithi na tanzu nyingine za fasihi zinazotokana na utungaji huburudisha, huliwaza na kufurahisha jamii.
· Utungaji hutumika kukuza lugha kwa njia ya mazungumzo au maandishi. Mzungumzaji na msikilizaji hupata ufundi wa kujieleza zaidi kupitia utungaji, hali kadhalika mwandishi na msomaji hupata ufundi wa kujieleza zaidi kupitia njia ya utungaji.
Kanuni za Utungaji bora
Utungaji bora ni lazima uzingatie kanuni zifuatazo:
· Matumizi mazuri ya nyakati: mfano, wakati uliopo, ujao na uliopita au hali timilifu.
· Matumizi mazuri ya lugha fasaha (lugha inayoeleweka).
· Mpangilio mzuri wa mawazo na mantiki, yaani kutochanganya mawazo, kutorudiarudia mawazo au kutosahau mawazo.
· Matumizi bora ya vituo na alama za uandishi.
· Matumizi bora ya sarufi ya lugha inayohusika.
· Utungaji bora hugawanyika katika sehemu kuu zinazobainisha muundo wa kazi yenyewe mf. Insha hugawanyika sehemu nne ambazo ni: Kichwa cha insha, Utangulizi, Kiini na Hitimisho
· Utungaji bora huwa na mifano ya kutosha.
Uandishi wa Insha
Insha ni utungo wenye sentensi nyingi zilizopangwa katika aya, zenye kuzungumzia mada moja. Kwa mfano, insha zinaweza kuwa zinazungumzia mada zifuatazo: Umuhimu wa Chakula Bora, Tiba Kutokana na Vyakula; Ujamaa ni Imani au Jamii Inakwenda Kombo.
Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa Insha.
Bila kujali aina ya insha inayoandikwa, yapo mambo kadhaa ya kuzingatia wakatiwa kuandika insha. Mambo hayo ni pamoja na:
(a) Kubaini mada ya kuandikia insha na kuielewa vyema.
(b) Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki
© Kutumia mtindo unaoendana na kusudi la insha. Kwa mfano, mtindo wa
masimulizi, unafaa kwa hadithi au insha zingine za kisanaa.
(d) Kutumia lugha fasaha na inayoeleweka
(e) Kufuata kanuni za uandishi. Kwa mfano, matumizi ya alama za uandishi,
aya, herufi kubwa na ndogo, n.k
(f) Kupanga insha katika muundo wake, yaani kichwa, utangulizi, kiini na
hitimisho.
Muundo Wa Insha
Insha hugawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni:
· Kichwa cha Insha
Kichwa cha insha huandikwa kwa herufi kubwa, katikati, juu ya insha. Hakipaswi kuzidi maneno matano na hupigiwa mstari.
· Utangulizi (Mwanzo)
Katika sehemu hii inampasa mwandishi atoe maelezo mafupi na maana ya habari aliyopewa.
· Kiini cha insha (Kati)
Inamlazimu mwandishi afafanue kwa mapana mada anayoishughulikia huku akitoa mifano hai inayoendana na hali halisi.
· Hitimisho (Mwisho)
Inampasa mwandishi kutoa mapendekezo (maoni) ya msingi au kusisitiza kwa ufupi yale aliyoyaelezea katika habari yenyewe.

NB: Hitimisho sio ufupisho wa hoja zilizojadiliwa katika sehemu ya insha
yenyewe.
Aina za Insha
Aina ya insha au jina la insha hujulikana kutokana na mawazo ya mwandishi. Kuna aina nyingi za insha lakini tunaweza kuziweka aina hizo katika makundi makuu mawili ya insha za hoja na insha za wasifu. Kila kundi kati ya makundi haya mawili kuna insha za kisanaa na insha zisizo za kisanaa.
Zingatia kielelezo kifuatacho
Insha za Kisanaa
Hoja
Insha zisizo za Kisanaa

Insha Insha za Kisanaa

Wasifu
Insha zisizo za Kisanaa

Insha za kisanaa hutumia vipengele mbalimbali vya fasihi katika kuwasilisha ujumbe - mfano nahau, methali, ,misemo au tamathali za semi huweza kutumika. Insha zisizo za kisanaa hazitumii lugha ya kifasihi katika kufikisha ujumbe.

Insha za wasifu huelezea sifa (uzuri au ubaya) za kitu, hali au mtu fulani. Insha za hoja ni insha ambazo hutetea mawazo ya aina fulani na kupinga mengine kwa uthibitisho uliodhahiri. Mfano wa insha za wasifu ni Uzuri wa bahari ya Hindi, Fahari ya Mlima Kilimanjaro, n.k. mfano wa insha za hoja ni: Ukimwi ni Ugonjwa Hatari, Uhuru wa Bendera, n.k.
Mfano wa Insha ya Wasifu
Atukuzwe Nyerere wa Tanzania
Nyerere wa Tanzania, kiongozi shujaa wa dunia – amepata kutukuka pande zote za dunia. Alizaliwa katika kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara. Alisoma elimu ya msingi katika shule ya Mwisenge – mojawapo ya shule za zamani sana hapa nchini. Alipata elimu ya sekondari huko Tabora. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kabla ya kwenda huko Uingereza kusomea shahada ya M.A.
Baada ya uhuru toka Uingereza, Mwalimu Nyerere alishughulika sana na suala la ukombozi wa Tanganyika na Afrika kwa ujumla. Alionesha jitihada za wazi kupambana na mabeberu wa Kiingereza hadi uhuru wa Tanganyika ukapatikana tarehe 9/12/1961. Tanganyika ikawa ya kwanza kupata uhuru wake ukilinganisha na nchi zote za Afrika ya Mashariki na kati – sifa kuu kwa Nyerere wa Tanganyika.
Nyerere alishirikiana na Karume kuziunganisha nchi hizo na kuzaa Tanzania – jina lililotumika na kuheshimiwa kote ulimwenguni. Wakati Nyerere akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar alitamka maneno ya hekima yafuatayo:
“Tumeamua kuziunganisha nchi zetu ili kuimarisha umoja wa Afrika. Naamini kuwa maadui wetu watachukia na kuhuzunika kwa kitendo hiki cha kishujaa tulichokifanya, lakini daima hatutaogopa chochote. Muungano wetu utadumu milele na milele. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika. Amina!”
Sifa ya pekee inayomtofautisha Mwalimu Nyerere unapomlinganisha na wanafalsafa wengine duniani kama vile Karl Marx na Mao ni kwamba yeye aliwapigania wanyonge wote kote ulimwenguni bila kujali ubaguzi wa rangi, kabila, taifa au bara. Aliwatetea wanyonge wa Afrika. Aliwapigania wanyonge wa Ulaya na Mashariki. Aliwapigania wanyonge wa bara la Asia. Hali kadhalika aliwapigania na kuwatetea wanyonge wa bara la Amerika ya Kusini. Hivyo ni sifa ya pekee inayofaa kumtofautisha na wanafalsafa wengine waliomtangulia.
Nyerere atatukuzwa daima kwa ushujaa wake. Alikuwa si kiongozi wa kujikombakomba kwa mataifa mengine ya kibeberu. Alipotishiwa au kuwekewa vikwazo/vitisho, alivunja mara moja uhusiano wa kidiplomasia na taifa linalohusika. Kwa mfano mwaka 1965 alivunja uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza baada ya nchi hiyo kuitangaza nchi ya Zimbabwe kama koloni lake la kudumu la Walowezi. Kitendo hiki kilimpatia sifa na heshima kubwa hapa Afrika na duniani kote – kwa wapenda amani.
Ingawa ni vigumu kuzitaja sifa zake mpaka mwisho, lakini sifa ya kupiga makelele katika majukwaa ya kimataifa haitaweza kusahaulika. Hakuwa msomi mkimya kama wasomi wa enzi hizi. Alitumia elimu yake ipasavyo kuitetea falsafa yake ya Haki na Usawa kwa Binadamu Wote katika majukwaa ya kimataifa.
Wananchi wa Uganda daima humkumbuka na kumtukuza kwa jinsi alivyotumia nguvu za kijeshi kuung’oa utawala wa kidikteta wa Nduli Idd Amini Dada. Wakikumbuka mateso waliyoyapata enzi za utawala huo, humtukuza na kumuenzi Nyerere usiku na mchana.
Nyerere hataweza kusahaulika kwa jinsi alivyopinga kitendo cha viongozi wachache wenye hila kuendelea kung’ang’ania kwenye madaraka. Alikuwa kiongozi wa kwanza hapa Afrika na pengine duniani kote kung’atuka kwenye kiti cha Urais. Alifanya hivyo kwa hiyari ili kutoa nafasi kwa wananchi wengine washike wadhifa huu nyeti hapa nchini kwetu.
Mwalimu Nyerere ni mwenzetu, ni rafiki yetu, ni mtu wa watu, ni baba wa taifa letu, ni babu yetu mwenye hekima na busara. Paji lake la uso lilijaa hekima na busara. Kinywa chake daima kilinena maneno ya hekima na busara. Fikra zake zitadumu milele kwenye vichwa vya wakulima, wasomi, wanafalsafa, mapadri, masheikh, wachungaji, watawa na hata kwenye bongo za waovu wa Tanzania daima watamkumbuka.
Kifo cha Mwalimu Nyerere kimeleta pengo kubwa kwa jamii yote ya wapenda amani kote ulimwenguni. Ingekuwa mbegu ya mmea tungeipanda sote tuendelee kuhekimika kutokana na hekima na busara zake.
Kifo cha Mwalimu Nyerere ni kama mwindaji asiye na silaha kwenye mwitu wenye wanyama wakali kama fisi, simba, ngiri, tembo, nyoka, nyati, n.k. Je, mwindaji atafanya nini?
Daima sifa na hekima za Mwalimu Nyerere zitukuzwe Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote.
Mfano wa insha ya hoja
Kijana wa leo nina balaa!!
Kilio, kilio, kilio kwa kijana wa leo, Afrika! Wakati vijana wengine wanapoombwa kujiunga na jeshi ili kujenga na kulinda nchi yao, siyo kwangu. Kwangu naburutwa msituni, kujiunga na jeshi kuendeleza vita ya wenyewe kwa wenyewe. Napigana na ndugu zangu ndani ya taifa moja ili matumbo machache yafaidi almasi, dhahabu, mafuta na maliasili nyingine. Naingizwa katika vita isiyo na maana yoyote kwangu.
Nikitaka kutafuta elimu, hakuna madarasa. Upepo umeezua paa la nyasi la shule yetu! Nikibahatika kupata kaelimu kadogo; chini ya mti, nazuiwa kufikiri zaidi. Naambiwa kuwa, Afrika hakuna kufikiri! Mtu mweusi hana fikra ila mtu mweupe ndiye mwenye fikra. Natakiwa nifuate fikra zake!
Nikitaka ajira, naambiwa uzoefu miaka mitano au kumi na zaidi. Uzoefu nitaupata wapi? Nikitamani kujiajiri mazingira hayaniruhusu: Umasikini, umasikini tena umasikini umenikumbatia!
Nikijiunga na siasa, wimbo maarufu kote ulimwenguni ni demokrasia. Demokrasia ina mizengwe, umajimbo, ukabila, udini, ubabe, rushwa, ubabaishaji, utapeli na kushindana bila kukubali kushindwa. Siasa barani kwetu ni kiini macho na matokeo yake ni ‘demoghasia’ isababishayo vifo. Ubinafsi umejaa! Kujipitishia marupurupu kibao! Ubaguzi! Majigambo! Dharau…..!
Nikitaka kusema, naambiwa mjinga, Nikidai haki, naambiwa madai yangu ni ya kijinga. Nalazimishwa kuandika barua ya kuomba msamaha na kuahidi kuwa sitadai haki tena! Nalazimishwa kuwa bubu. Kijana msomi nanyimwa uhuru wa kutoa mawazo yangu mbele ya jumuiya yangu. Kijana msomi nafungwa mdomo. Kijana msomi kukaa na kunyamaza kimya ni usaliti. Usaliti kwa jamii ya walipa kodi ambao pesa zao zimenisomesha hadi kuitwa msomi. Kijana msomi, kutofikiri ni dhambi nyekundu pyuuu!- isiyosameheka. Msomi kutofikiri ni kifo cha kifikra kwangu mimi kijana wa Kiafrika.
Chochote ninachotaka kufanya kinanikatisha tamaa. Nikiwa ‘deiwaka’ mpiga debe, kila siku nitaamkia korokoroni! Nikitaka kujiburudisha na gongo au viroba - ni kifo cha ajabu. Nikibugia unga – kwangu ni kifo cha mende wekundu! Nikijiingiza kwenye ukahaba, natozwa kodi ya maendeleo! Nikitaka kuwa “changudoa”, UKIMWI unaniwinda kama mamba awindavyo viumbe baharini! Sasa nifanye nini? Balaa kubwa kwangu!
Nikiamua kuokoka, wokovu hauonekani. Nimebaki njia panda. Mchungaji amekuwa mwongo, katu hasemi ukweli. Ananilaghai kuwa wokovu upo karibu kuingia badala ya kuniambia kweli wokovu umekwishatoweka. Naambiwa kuwa nijiwekee hazina mbinguni ambako kutu na wadudu hawataharibu mali yangu…Huu ni utapeli.
Ingekuwa vizuri kama ningeelezwa wazi jiwekee akiba tumboni mwa sheikh au tumboni mwa mchungaji au tumboni mwa padre! Naambiwa kuwa toeni ulichonacho utabarikiwa badala ya kuambiwa kuwa kitayabariki matumbo ya wachache!
Nakumbuka wakati mama yangu alipokuwa mwalimu katika shule ya msingi ya Mabonde Kuinama, aliniambia kwamba, urithi wa utamaduni wetu ni mila na desturi za Afrika. Lakini siku hizi sivyo. Siku hizi naambiwa kuwa urithi wa kizazi kipya ni bia aina ya “Safari Larger”.
Kijana wa sasa naangalia wizi wanaofanyiwa watu maskini lakini sisemi chochote. Najinyamazia kimya. Wizi umo makanisani, misikitini, Ikulu, mahakamani na hata bungeni. Lengo ni kuwanyanyasa, kuwadhulumu, kuwaonea, kuwanyonya na kuwadhalilisha wanyonge. Hakika kunyamaza kwangu ni usaliti. Nimeitambua nafasi yangu. Naahidi kupambana hadi kufa na kupona.
Uandishi wa barua na kadi za mialiko
Kuna aina mbalimbali za barua. Aina hizo hugawanywa katika makundi makuu mawili ambayo ni Barua za kirafiki/kindugu na Barua rasmi.
(a) Barua za Kirafiki/Kindugu
Hizi ni barua zinazoandikwa kwenda kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa madhumuni mbalimbali kama vile:
- Kusalimiana
- Kujulishana maisha yetu ya kila siku
- Kuomba msaada au kutoa shukrani kwa kutimiziwa maombi yetu.
- Kutoa hongera, rambirambi, pongezi, n.k.
Sehemu za Barua za Kirafiki/Kindugu
v Anuani ya Mwandishi
Huandikwa kwenye pembe ya kulia ya karatasi. Anuani hii ndiyo hutumiwa na mwandikiwa wakati wa kujibu barua aliyoipokea na pia hutambulisha maskani ya mwandishi wa barua kwa wakati huo. Kwa hiyo, ni wajibu wa mwandishi kuandika anuani yake vizuri. Ni lazima iandikwe waziwazi.

v Tarehe
Hii huandikwa mara baada ya anuani ya mwandishi. Huandikwa ili kumjulisha mwandikiwa barua imeandikwa lini na kama imefika kwa wakati au imechelewa. Zipo njia mbalimbali za kuandika tarehe, nazo ni:
- 20.9.2017
- 20/9/2017
- 20-9-2017
- 20 Septemba, 2017
- Septemba 20, 2017


v Mwanzo wa barua
Barua za kirafiki/kindugu huanza kama ifuatavyo:
- Baba mpendwa,
- Mpendwa baba,
- Mwanangu mpendwa,
- Mama mpenzi, n.k.

v Barua yenyewe
Hii ni sehemu muhimu sana. Sehemu hii ndiyo inayomfanya mwandikiwa aelewe kusudi la mwandishi. Sehemu hii iandikwe vizuri ili barua ieleweke kwa urahisi.

v Mwisho wa barua
Mwisho wa barua ni sehemu inayostahili kuandikwa vizuri. Njia zifuatazo ni baadhi ya zile zitumikazo kumalizia barua ya kindugu.
- Mwanao akupendaye.
- Wako wa moyoni.
- Rafiki yako akupendaye.
- Wako akupendaye.
- Wasalaam, baba yako, n.k.

v Jina la Mwandishi
Ni vizuri kuandika jina lako mwishoni mwa barua ili yule unayempelekea afahamu barua imetoka kwa nani.

Mfano wa barua ya kirafiki

Shule ya Sekondari Mbezi Beach,
S.L.P 60213,
Dar Es Salaam.
03/07/2017.
Mpendwa,
Salaam sana. Natumai u mzima pamoja na jamaa na marafiki wa hapo nyumbani. Nami ni mzima na ninaendelea na masomo yangu vizuri hapa shuleni. Napenda kukujulisha kuwa maendeleo yangu kimasomo hapa shuleni ni mazuri sana. Katika mtihani wa kumaliza mwaka wa pili nimeshika nafasi ya pili kati ya wanafunzi 195 wa kidato cha tano. Nimeamua kusomea mchepuo wa biashara ili hatimaye niwe mchumi wa nchi yetu hivyo naomba tuzidi kuombeana heri.

Pamoja na mafanikio hayo yote, kuna tatizo kubwa sana ambalo linazidi kuniandama hapa shuleni. Tatizo hili linanikosesha kabisa raha, kila wakati huwa ninahuzunika. Tatizo hili huwa ni la umasikini. Sina hata shilingi tano ya kununulia kipande cha muhogo. Hivyo, naomba uuze yule jogoo mkubwa unitumie pesa haraka iwezekanavyo.

Wasalimie wote wanaonifahamu hapo kijijini. Msalimie sana shangazi wangu Lilian Joackim.
Wako akupendaye,
Haidari Hamisi.

(b) Barua Rasmi
Kwa kawaida barua rasmi huandikwa kwa makusudi mbalimbali kama vile, kutoa taarifa za tukio fulani, kuomba kazi, kuagiza vifaa au vitu, kumwalika kiongozi katika shughuli maalumu, kutoa taarifa ya kushindwa kufika mkutanoni, n.k.

Barua rasmi zipo za aina nyingi, lakini zinaweza kugawanywa katika makundi matatu makubwa yafuatayo:
- Barua za kuomba kazi
- Barua za kutoa taarifa
- Barua za kuagiza au kupokea bidhaa/vitu.
Sehemu za barua rasmi
(i) Anuani ya mwandishi
Anuani hii huandikwa pembe ya juu kulia ili kutambulisha maskani ya mwandishi na pia hutumiwa na mwandikiwa wakati wa kuijibu barua husika inapobidi.

(ii) Tarehe
Huandikwa chini ya anuani ya mwandishi ili kumjulisha mwandikiwa kama barua hiyo imefika mapema au imechelewa.

(iii) Kumbukumbu namba
Barua rasmi huwa na kumbukumbu namba. Huu ni utambulisho maalumu wa barua husika. Kumbukumbu namba aghalabu huwa ni kifupi cha jina la taasisi inakotoka barua hiyo, kule inakokwenda, hiyo ni barua ya ngapi na mwaka husika. Mf: Mbss/crdb/02/17

(iv) Anuani ya mwandikiwa
Anuani hii hutanguliwa na cheo cha mwandikiwa na huwekwa upande wa kushoto chini ya kumbukumbu namba. Nafasi ya mstari mmoja au zaidi huweza kurukwa baina ya kumbukumbu namba na anuani ya mwandikiwa.

(v) Mwanzo wa barua
Sehemu hii huandikwa chini ya anuani ya mwandikiwa. Ni heshima kutaja cheo cha mwandikiwa mwanzoni mwa barua ya namna hii, kwa mfano Ndugu Katibu, Ndugu Ofisa Mifugo, n.k.

(vi) Kichwa cha barua
Kichwa cha barua hutaja kwa ufupi jambo linalohusu barua hiyo. Kichwa cha barua huandikwa waziwazi katikati ya barua mara baada ya mwanzo wa barua. Ni muhimu kiwe kifupi na chenye kueleweka waziwazi. Hufaa zaidi kikiandikwa kwa herufi kubwa na kupigiwa mstari. Hakipaswi kuzidi maneno matano.

(vii) Barua yenyewe
Sehemu hii huandikwa mambo yote muhimu kuhusu barua yenyewe. Barua yenyewe iwe fupi na yenye taarifa za lazima tu. Uanzaji wa barua yenyewe umrejeshe msomaji kwenye mada ili kufupisha maelezo mengi kama vile kwa kusema:
- Mada tajwa hapo juu inahusika
- Rejea barua yako ya tarehe…..yenye Kumb. Na….
- Husiana na mada tajwa hapo juu, n.k.

(viii) Mwisho wa barua
Mwisho wa barua huwa ni tamko la heshima la kumalizia barua. Mara nyingi mwisho unaotumika katika barua rasmi ni kama vile:
- Wako mtiifu,
- Wako katika ujenzi wa taifa,
- Wako katika kazi, n.k.

(ix) Saini na jina la mwandishi
Mwisho wa barua mwandishi hupaswa kutia saini na jina lake kama utambulisho wake juu ya kilichoandikwa. Saini hupaswa kutiwa kwa mkono.

(x) Cheo cha mwandishi
Baada ya jina mwandishi hupaswa kuandika cheo chake. Cheo kinaweza kuwa:
- Mwanakijiji
- Muombaji
- Mwalimu Mkuu
- Afisa Mtendaji, n.k


Aina za Barua Rasmi
1. Barua ya Kuomba Kazi
Barua ya kuomba kazi inahitaji uangalifu sana katika sehemu ya barua yenyewe. Barua hii inatakiwa iandikwe kwa umakini na ujuzi mwingi. Katika barua hii kuna mambo makuu manne ambayo ni: kutaja kazi unayoomba, jinsi ulivyopata taarifa, elimu, ujuzi na uzoefu, maelezo binafsi na wadhamini.

Mfano wa barua ya kuomba kazi:
Kijiji cha Mto wa Mbu,
S.L.P 4507,
Arusha.
04/7/2017
Meneja wa Kiwanda,
Kiwanda cha Kusindika Matunda,
S.L.P 0717,
Iringa.
Ndugu,
YAH : OMBI LA KAZI YA UKARANI
Husika na kichwa tajwa hapo juu. Ninayo heshima kuomba kazi ya ukarani katika kiwanda chako kama ilivyotangazwa kupitia gazeti la “Sanifu” Uk. 3 la tarehe 20/6/2017.
Mimi nilisoma katika kituo cha Elimu ya Watu Wazima huko Mufindi. Baadaye nilijiunga na masomo kwa njia ya posta na kuhitimu kwa ufaulu wa masomo ya Kiswahili, Siasa na Kiingereza.
Nina umri wa miaka 45, nimeoa na nina watoto wanne. Mimi ni mwanakijiji wa kijiji cha Magadini. Napendelea michezo na kazi za mikono. Ninaweza kusoma na kuandika vizuri na ninayo hati nzuri.
Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Mufindi na msimamizi wa masomo kwa njia ya posta anaweza kutoa taarifa zaidi juu ya uwezo wangu.
Nitashukuru sana iwapo ombi langu litafikiriwa na kupokelewa vema.
Wako mtiifu,
(Saini)
Matatizo Hayaishi
Mwombaji
Barua ya kupitia kwa:
Iwapo barua itapaswa kupitishwa na mtu zaidi ya mmoja kutokana na mamlaka za kiutawala na utambuzi mwandishi atapaswa kuandika anuani za wale wanaopaswa kuiona barua hiyo kwa kuanza na anuani ya yule atakayeiona mwisho.
Mfano:
Kijiji cha Mto wa Mbu,
S.L.P 4507,
Arusha.
04/7/2017
Meneja wa Kiwanda,
Kiwanda cha Kusindika Matunda,
S.L.P 0717,
Iringa.

K.K
Afisa Rasilimali Watu,
Kiwanda cha Kusindika Matunda,
S.L.P 0717
Iringa
Ndugu,
YAH : OMBI LA KAZI YA UKARANI
Husika na kichwa tajwa hapo juu. Ninayo heshima kuomba kazi ya ukarani katika kiwanda chako kama ilivyotangazwa kupitia gazeti la “Sanifu” Uk. 3 la tarehe 20/6/2017.
Mimi nilisoma katika kituo cha Elimu ya Watu Wazima huko Mufindi. Baadaye nilijiunga na masomo kwa njia ya posta na kuhitimu kwa ufaulu wa masomo ya Kiswahili, Siasa na Kiingereza.
Nina umri wa miaka 45, nimeoa na nina watoto wanne. Mimi ni mwanakijiji wa kijiji cha Magadini. Napendelea michezo na kazi za mikono. Ninaweza kusoma na kuandika vizuri na ninayo hati nzuri.
Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Elimu ya Watu Wazima cha Mufindi na msimamizi wa masomo kwa njia ya posta anaweza kutoa taarifa zaidi juu ya uwezo wangu.
Nitashukuru sana iwapo ombi langu litafikiriwa na kupokelewa vema.
Wako mtiifu,
(Saini)
Matatizo Hayaishi
Mwombaji

2. Barua ya kutoa taarifa
Barua hizi huandikwa kwa lengo la kutoa taarifa juu ya jambo, tukio au mtu. Taarifa huweza kutolewa kwenye taasisi fulani kama kituo cha polisi au ofisi yoyote ya umma.

Mfano wa barua ya kutoa taarifa
Kijiji cha Jangwani,
S.L.P 1045,
Mto wa Mbu
10/7/2017.
Bwananyama wa Wilaya,
Wilaya ya Monduli,
S.L.P 1045,
Arusha.
Ndugu,
YAH: TATIZO LA SIMBA KIJIJINI
Husika na mada tajwa hapo juu. Ninasikitika kukutaarifu kuwa, hapa kijijini kwetu amezuka simba anayewinda watu. Ni simba jike na watoto watatu na ameonekana mara tatu hapa kijijini.
Simba huyo huingia hapa kijijini kutoka katika msitu wa hifadhi ya taifa ambapo si ruhusa kuweka mitego.
Nashukuru ikiwa utatushauri haraka jambo la kufanya mara upatapo barua hii.
Wako katika kazi,
(Saini)
Rogathe Kimario
Mtendaji wa Kijiji
3. Barua ya Mwaliko
Barua za aina hii huandikwa kwa viongozi mbalimbali kwa lengo la kuwaalika katika shughuli mbalimbali kama mahafali, uzinduzi, ufunguzi, n.k

Mfano wa barua ya mwaliko
Shule ya Sekondari Manyara,
S.L.P 46,
Arusha.
15/7/2017.
Mkuu wa Wilaya,
Wilaya ya Monduli,
S.L.P 12,
Arusha.
Ndugu,
YAH: MWALIKO WA KUKABIDHI VYETI
Husika na kichwa cha barua hapo juu. Ninakualika uwe mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita yatakayofanyika hapa shuleni siku ya tarehe 20/7/2017 kuanzia saa saba za mchana hadi saa 12 jioni. Pia utatunuku vyeti vya kuhitimu kwa wahitimu 600 katika sherehe hiyo.
Nitashukuru sana iwapo ombi letu litakubaliwa.
Wako katika ujenzi wa taifa,
(Saini)
Gambuzi Peter
Mkuu wa Shule


4. Barua ya kuagiza/kupokea bidhaa (Barua za kibiashara)
Barua hizi huandikwa kwa lengo la kuagiza bidhaa au kukiri kupokea bidhaa zilizotumwa.

Mfano wa barua ya kuagiza bidhaa
Kijiji cha Mkwawa,
S.L.P 20,
Iringa.
12/7/2017
Meneja wa Kiwanda,
Kiwanda cha Zana za Kilimo Mbeya,
S.L.P 44,
Mbeya.
Ndugu,
YAH: AGIZO LA ZANA ZA KILIMOHusika na kichwa cha barua hapo juu. Tunaomba ututumie zana za kilimo, kwani tunakusudia kuanzisha mradi wa kilimo cha mahindi hapa kijijini. Zana tunazohitaji kwa ajili ya mradi huu ni :
- Majembe – 6
- Mapanga – 10
- Mashoka – 6
- Slesha – 20
- Toroli – 2
Tunaomba utume kwa basi la Simama Trans linalofanya safari zake kila siku hapa Iringa. Kabla ya kutuma, tuandikie kutuarifu tarehe utakayotuma. Malipo yatalipwa kwa hundi.
Wako katika ujenzi wa taifa,
(Saini)
Nyanya Kitunguu
Mratibu wa Mradi
5. Kadi ya Mwaliko
Kadi ya mwaliko huandikwa kwenye karatasi maalumu inayoitwa kadi. Kadi ya mwaliko huwa na mambo yafuatayo:
- Jina la mwalikaji na anuani
- Jina la mwalikwa
- Lengo la mwaliko
- Mahali pa tukio
- Muda wa kukutana
-
Familia ya Bw. & Bibi Majaliwa Maisha wa S.L.P 007 Dar es Salaam, wanayofuraha kukuali/kuwaalika Bw. & Bibi./ Bw./ Bi./ Prof./ Dkt./ Mch./ Sheikh./……………. kwenye mahafali ya kijana wao mpendwa ………….yatakayofanyika shuleni kwao siku ya tarehe 10/7/2017 na baadaye kwenye tafrija fupi nyumbani kwao kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.
Kufika kwako ndiyo mafanikio ya tafrija yetu.
Majibu kwa wasiofika
SIMU: 0717104507
Mawasiliano kwa ajili ya majibu


ZINGATIA: Kadi ya mwaliko huweza kujibiwa kwa kutumia muundo wa barua ya
kirafiki au barua rasmi.

6. Barua ya gazetini
Barua za magazetini ni zile zinazoandikwa na wasomaji wa magazeti fulani fulani kwa mhariri. Barua hizi huwa na madhumuni anuai ambayo huwa na nia mbalimbali kama vile:
- Kutoa pongezi
- Kufichua maovu
- Kutoa maoni na mapendekezo
- Kupinga madai ya barua ya awali iliyoandikwa gazetini humo kuhusiana na mada fulani
- Kuunga mkono madai ya barua fulani iliyoandikwa gazetini
- Kulalamikia hali fulani, kwa mfano usalama wa nchi
- Kuwafahamisha wasomaji kuhusu jambo fulani, kwa mfano umuhimu wa kompyuta katika shule za sekondari, n.k

Muundo wa barua ya gazetini
- Kichwa cha barua - huandikwa mwanzoni kabisa na huandikwa kwa herufi kubwa na kupigiwa mstari au wino mzito
- Mwanzo wa barua – mf: ndugu mhariri
- Barua yenyewe – huwa na ufafanuzi wa hoja zenye ukweli na ushahidi wa kutosha.
- Mwisho wa barua – mara nyingi mwisho wa barua za magazetini huwa na ombi, maoni au mapendekezo.
- Jina la mwandishi na anuaini – huandikwa chini, upande wa kushoto.
- Tarehe – huandikwa baada ya jina na anuani (japo si lazima)


Mfano wa barua ya gazetini:
Nakerwa na Uchafuzi Dar es Salaam
Mhariri,
Miongoni mwa mambo yanayonikera katika Jiji la Dar es Salaam ni uchafu uliokithiri huku viongozi wake wakionesha kushindwa kabisa kukabiliana na hali hiyo.
Ndugu mhariri, nimekuwa nikitembelea maeneo ya Kinondoni shamba, Kariakoo, Tandale, Manzese, Buguruni pamoja na Vingunguti kutokana na shughuli zangu za kutembeza bidhaa lakini maeneo haya kwa kweli yanatia mashaka.
Kumekuwepo na maji machafu yanayotiririka kutoka kwenye vyoo pamoja na lundo la takataka barabarani. Jambo hili kwa kweli inaharibu taswira ya Jiji hili.
Kwa bahati mbaya viongozi wa mitaa pamoja na wajumbe wamekuwa hawawajibiki katika kuhakikisha mazingira haya yanaboreshwa na kuwa masafi.
Matokeo yake kumekuwepo na ongezeko la watu wanaopata maradhi ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kuumwa tumbo, ukurutu na kuenea kwa harufu mbaya.
Nakumbusha mamlaka husika kwamba, kukosekana kwa afya njema ni miongoni mwa sababu ya kushindwa kuzalisha na hivyo kudhoofisha uchumi wa nchi.
Viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wasaidizi wao ambao ni wajumbe wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi.
Kwa kufanya hivyo wanaweza kuaminika kwa wananchi na hivyo kuheshimiwa kama viongozi na hiyo ndiyo kazi ya uongozi inavyopaswa kuwa.
Ni wajibu si kwa viongozi serikalini pekee lakini hata kwa wananchi ili kuhakikisha mazingira wanayoishi yanakuwa safi jambo litakalowezesha kusaidia kuepuka maradhi na mambo mengi yanayotokana na uchafu.
Pamoja na hivyo, halmashauri zinapaswa kutunga sheria ndogo ndogo zinazolenga kutunza usafi wa mazingira na kuzisimamia.
Rashi S. Mbonde
[email protected]
Ilala, Dar es Salaam

(Kutoka gazeti la MAWIO, Alhamisi, Agosti 6-12, 2015 Uk.14)

7. Simu ya Maandishi
Simu za maandishi ni mojawapo ya mawasiliano ya haraka baina ya watu. Waandikiwa hupata taarifa haraka iwezekanavyo ukilinganisha na barua za kawaida. Taarifa ya simu ni fupi lakini huwa na ujumbe ulio wazi na unaoeleweka. Ufupi wa simu za maandishi unatokana na gharama kubwa za malipo kwa sababu gharama za simu hulipwa kulingana na idadi ya maneno yanayoandikwa.
Barua za simu zipo za aina mbalimbali kama vile:
· Barua za simu ya kawaida
· Barua za simu ya haraka
· Barua za simu ya kupeleka fedha
Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa barua za simu
(i) Anuani ya anayepelekewa taarifa
Anuani ya simu ya maandishi lazima iwe kamili na ya waziwazi ili kuiwezesha barua hiyo kupelekwa haraka iwezekanavyo bila ya matatizo. Anuani ya mji ni lazima iwe na jina la mtaa na kama inawezekana namba ya nyumba. Vilevile jina la ofisi ya simu iliyo karibu na mahali simu hiyo inakopelekwa.
(ii) Taarifa au ujumbe wenyewe
Hapa ndipo penye kiini cha simu. Habari ielezwe kwa ufupi sana lakini ieleweke vizuri. Epuka mambo yasiyo ya lazima.
(iii) Jina la mwandishi au mtuma simu
Jina la mwandishi huandikwa kwa ukamilifu wake ili kumjulisha mwandikiwa barua imetoka kwa nani.
Alama za uandishi hazitumiki isipokuwa kama nazo ni sehemu ya neno.
Kumbuka: Ni muhimu kuandika maneno yote kwa herufi kubwa ili kurahisisha usomaji. Barua ya simu hutumika hasa kwa ajili ya mambo ya haraka sana na muhimu. Simu huandikwa kwenye karatasi maalumu. Karatasi hizo hupatikana posta.


Hakuna barua ya simu ya aina yoyote ambayo itasafirishwa bila ya kulipiwa gharama ya kuipeleka simu hiyo. Hivyo, barua ya simu huwa fupi ili kuepuka gharama za utumaji.
Mfano wa simu ya maandishi

JUMA ALI SLP 20 MAKUYUNI
FIKA HARAKA BABA MAHUTUTI
FARIDA BAKARI8. Uandishi wa Matangazo
Uandishi wa matangazo ni shughuli ya kampuni, serikali au mtu binafsi ya kusambaza habari. Kampuni huweza kutangaza bidhaa zake, nafasi za kazi, mabadiliko fulani katika kampuni au shughuli muhimu katika kampuni. Matangazo ni habari zinazowekwa wazi kwa nia ya kupitishwa kwa hadhira fulani. Matangazo huhusu jambo fulani kama vile mkutano, mashindano, harambee, n.k.

Vyombo vya habari kama vile magazeti, televisheni hutumiwa. Matangazo pia huweza kuwekwa kwenye mabango. Matangazo huweza kuwa na habari za kutoa onyo au kufahamisha. Kwa mfano kampuni huweza kuwatangazia wanunuzi wake kuhusu hatari ya kununua bidhaa zisizo na chapa ya kampuni hiyo. Tahadhari, onyo, ilani na notisi ni aina za matangazo yanayotekeleza majukumu mbalimbali.

Sifa za matangazo
Matangazo hudhamiriwa kuwanasa wasomaji/wasikilizaji. Kwa hiyo, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
v Yawe mafupi – matangazo marefu huchosha na kusahaulika haraka.
v Yatumie lugha yenye mvuto na sahihi inayoeleweka.
v Yabandikwe sehemu za wazi ili watu wayasome kwa urahisi
v Kwa kawaida huandikwa kwa herufi kubwa au wino mzito unaoweza kuvuta makini ya watu.
v Huweza kuwa na picha ili kuongeza mvuto.
Matangazo huweza kuwa ya aina mbalimbali kulingana na majukumu yake. Zifuatazo ni baadhi ya aina za matangazo:
· Matangazo ya biashara
· Matangazo ya tahadhari
· Matangazo ya taarifa za habari
· Shughuli za kampuni
· Shughuli za serikali
· Kuenea kwa magonjwa, n.k
Mfano:

KAMPUNI YA KAMBI YA UUZAJI WA MASHAMBA
MASHAMBA YANAUZWA BEI NAFUU!! SHILINGI 200,000
KWA EKARI MOJA! SEHEMU CHACHE ZIMESALIA
NAMBA YA SIMU : 0717104507
CHAKUBANGA

DHIMA YA MATANGAZO KATIKA JAMII
(a) Kutangaza bidhaa mbalimbali ili kukuza soko la bidhaa hizo.
(b) Kutangaza ni njia mojawapo ya kuwasiliana na njia hii inaashiria ustaarabu wa
kupeana taarifa mapema kabla ya tukio linalokusudiwa kutekelezwa siku za
usoni.
© Kuelimisha jamii, matangazo hutumika kama vitanabaishi vyenye kutoa
tahadhari, maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali. Tumepata kusikia na kusoma
matangazo yanayohusu UKIMWI, malaria, wizi wa nyaya za simu na umeme.
Hii ni mifano ya matangazo ambayo dhima kubwa ni kuelimisha jamii juu ya
hayo yaliyotajwa.
(d) Kutangaza husaidia kuboresha shughuli za kiuchumi kama vile kufahamisha
jamii juu ya bidhaa mpya zilizotoka, huduma mbalimba zinazotolewa, mahali
wanapoweza kupata bidhaa au huduma hizo na mengineyo mengi yanayohusu
masoko na ongezeko la ziada kutokana na biashara. Kwa ujumla, lengo la
kutangaza ni, kushawishi, kuburudisha, kuonya, kutoa taarifa, kuuza bidhaa au
kutoa huduma, n.k
Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa matangazo
(a) Kichwa cha habari, kiandikwe kwa herufi kubwa
(b) Kutaja aina ya biashara (matangazo ya biashara)
© Kutaja aina ya bidhaa (matangazo ya biashara)
(d) Kutaja mahali inapopatikana hiyo bidhaa au huduma
(e) Kutaja njia za mawasiliano.
Uandishi wa matangazo ya biashara magazetini
Tangazo linapaswa kuwa na mambo yafuatayo:
(a) Kichwa cha tangazo ambacho huandikwa kwa herufi kubwa
(b) Kutaja aina ya biashara inayotangazwa
© Kutaja aina ya bidhaa unazouza na bei zake
(d) Kutaja mahali inapotolewa huduma husika
- mji
- mtaa
- kijiji
- kata, n.k
(e) Kutaja njia za mawasiliano
- kwa barua
- kwa simu
- kwa nukushi
- kwa wavuti, n.k
Mfano
9. Uandishi wa Hotuba
Hotuba ni maelezo ambayo hutolewa na mtu mbele ya watu. Hutolewa kwa madhumuni maalumu. Kwa mfano, hotuba inaweza kutolewa kwa madhumuni ya kuhimiza kazi, kufanya kampeni fulani au kutoa taarifa fulani kwa watu.
Sifa za hotuba
· Ukweli wa jambo linaloelezwa
· Ufasaha wa lugha
· Nidhamu ya mzungumzaji mbele ya watu
· Mantiki nzuri
· Sauti ya kusikika
Aina za hotuba
v Mahubiri: hizi ni hotuba za mafundisho ya kidini, hutolewa kanisani, msikitini au kwa njia ya redio na televisheni.
v Hotuba za kisiasa na Kiserikali: hizi ni hotuba za matangazo ya taarifa za kiserikali na chama, za kisiasa, kuhimiza na kualika watu kutenda jambo fulani, n.k
v Mihadhara au masomo ya darasani: hizi ni hotuba au mafundisho ya mwalimu shuleni hasa anapofundisha kundi kubwa la wanafunzi na hasa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Muundo wa hotuba
Muundo wa hotuba huwa na mwanzo, utangulizi, kati na mwisho.
Mfano:
Mwanzo – Mwanzo wa hotuba huwa na salamu.
Mzungumzaji: - Vijana safiiii!
Wasikilizaji: - Safiii!
Mzungumzaji: - Elimu juuuu!
Wasikilizaji : - Juuu!
Hii ni sehemu muhimu sana kwa ajili ya kuwaandaa wasikilizaji kuwa makini ili waweze kusikiliza yale yatakayotolewa kwenye hotuba na mzungumzaji.
Utangulizi
Huwa na utambulisho kulingana na vyeo. Mfano: “Mheshimiwa mgeni rasmi, ndugu wananchi, mabibi na mabwana…….”
Licha ya utambulisho, utangulizi huwa na shukrani pamoja na muhtasari wa hotuba itakayotolewa.
Kati
Baada ya utangulizi, kiini cha hotuba hufuata. Kiini ndicho hutoa ujumbe kwa wasikilizaji na ndiyo sehemu muhimu sana katika hotuba. Sehemu hii mtoa hotuba hueleza yale yote yaliyomsukuma kutoa hotuba hiyo.
Mwisho
Hapa huwa ni hitimisho, muhtasari wa yaliyoelezwa kwa ajili ya kusisitiza, shukrani na maagizo.
Mfano wa hotuba
HOTUBA YA MGENI RASMI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. CHARLES M. KITWANGA, MB AKIFUNGUA KIKAO CHA KAZI CHA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI UKUMBI WA ‘JULIUS NYERERE INTERNATIONAL CONVENTION CENTRE’, DAR ES SALAAM TAREHE 18 – 19 FEBRUARI 2016

Inspekta Jenerali wa Polisi, Ndugu Ernest Jumbe MANGU,
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdurahman KANIKI,
Makamishna wa Polisi,
Naibu Makamishna wa Polisi,
Wajumbe wa Mkutano,
Waandishi wa Habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Habari za asubuhi!
Heri ya Mwaka Mpya!
Napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo hii. Pili, natumia fursa hii kumshukuru Inspekta Jenerali wa Polisi ndugu Ernest Mangu kwa kunipa heshima hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika Kikao hiki muhimu. Kupitia hafla hii ninapata fursa ya kuzungumza na viongozi wote waandamizi wa Jeshi la Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi ambao ni wasimamizi wakuu wa kazi za Polisi. Ninawapongeza sana kwa utaratibu huu mliojiwekea wa kukutana kila mwaka kwa ajili ya kufanya tathimini lakini pia kuweka mikakati ya namna ya kuboresha huduma zenu kwa jamii pamoja na jinsi ya kuzidi kuboresha Jeshi la Polisi nchini.
Ndugu Wajumbe,
Ni matumaini yangu kuwa kikao hiki kitakuwa tofauti na vikao vilivyopita kutokana na kasi kubwa ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Falsafa yake ya ‘HAPA KAZI TU’. Ni lazima mbadilishe mtazamo na kufanya kazi kwa kasi inayoendana na Serikali hii. Fanyeni tathimini ya tulikotoka, upungufu, changamoto na fursa zilizopo ili kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi. Ni muhimu kupanga mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa kuzingatia changamoto zilizopo na upungufu mliouona kwa mustakabali wa amani na usalama wa taifa letu. Kukiwa na usalama, shughuli za kiuchumi zitafanyika kikamilifu na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Aidha, usalama wa nchi yetu utazidi kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini na kuongeza ajira nchini.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kuangalia tu aina ya wajumbe wa kikao hiki, nimeridhika kuwa Kikao Kazi hiki ni muhimu sana kwa kuwa nyinyi ndiyo msingi na dira ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini. Maamuzi yenu mtakayoyafanya kwenye kikao hiki na mkiamua kuyatekeleza kwa dhati taifa litakuwa limepiga hatua kubwa katika kukabiliana na wimbi la uhalifu nchini. Nimeambiwa kuwa kaulimbiu ya kikao hiki ni ‘Badilika kifikra, acha kufanya kazi kwa mazoea’. Kaulimbiu hii ni nzuri na ya maana kama mtaamua kuitekeleza kwa vitendo. Malalamiko ya Wananchi dhidi ya utendaji kazi wa Askari Polisi yatapungua kwa kiasi kikubwa sana.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kuwa hiki ni kikao changu cha kwanza kukutana na viongozi wote wa Jeshi la Polisi wa nchi nzima, nitumie fursa hii kutoa pongezi za dhati kwenu kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu. Mlisimamia kwa weledi wa hali ya juu sana Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani katika muda wote wa mchakato. Mlisimama imara kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano kwa watanzania wote. Hongereni sana kwa kazi nzuri.
Ndugu Wajumbe,
Pamoja na pongezi hizo, nafahamu kuwa zipo changamoto kadhaa za kiuhalifu ambazo ziliripotiwa katika kipindi kilichopita. Takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2015 makosa makubwa yaliyoripotiwa yalikuwa 68,814 ukilinganisha na makosa 70,153 yaliyoripotiwa mwaka 2014 ambayo ni pungufu ya makosa 1,339 sawa na asilimia 1.9 %. Kwa upande wa makosa madogo mwaka 2015 yaliripotiwa makosa 450,389 ukilinganisha na makosa 458,422 yaliyoripotiwa mwaka 2014 ambayo ni upungufu wa makosa 8,033 sawa na asilimia 1.8%.
Kutokanana takwimu hizo niwapongeze sana kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa kipindi cha mwaka jana, na niwasihi muongeze nguvu zaidi katika kupambana na uhalifu huku tukijikita katika kuzuia zaidi kuliko kusubiri uhalifu utokee.
Aidha, nawakumbusha kuwa katika kuhakikisha kuwa hili linafanikiwa ni lazima kujenga mahusiano mazuri na jamii kwani wao ndio hasa wahusika na waathirika wa uhalifu na wanawafahamu wahalifu kwa kuwa ni sehemu ya jamii. Mahusiano mazuri na jamii yatasaidia upatikanaji wa taarifa kwa wakati na hivyo kuwezesha askari wetu kushughulikia matukio ya kihalifu kwa wakati, weledi na ufanisi.
Ndugu Wajumbe,
Naelewa changamoto zinazotokana na upungufu wa vitendea kazi, nyumba, maslahi yasiyotosheleza kwa maafisa na askari, uhaba wa taaluma katika mafunzo na askari kuishi nje ya kambi. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia kwamba Serikali itaongeza jitihada ya kuliwezesha Jeshi la Polisi na askari kwa vitendea kazi vya kisasa kwa kadri uwezo wa bajeti utakavyoruhusu. Tutaendelea kuwajengea uwezo na maarifa ya kiutendaji kwa kuwaelimisha watendaji ili waendane na wakati wa sasa wa sayansi na teknolojia. Ni matarajio yangu kwamba mtatumia fursa zilizopo katika kutatua matatizo yanayolikabili Jeshi letu la Polisi, wakati jitihada kama nilivyoeleza hapo juu zinafanyiwa kazi kulingana na uwezo wa kifedha wa serikali. Aidha, napenda kusisitiza kwamba hatuna budi kutunza vizuri vifaa vilivyopo ili hivi vichache tulivyonavyo tuvitumie kwa muda mrefu zaidi. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha matumizi bora ya magari, nyumba, vifaa vya ofisini, matumizi ya umeme na maji katika makazi na ofisi. Ni muhimu sana kulisimamia hili ili kuepusha gharama zisizo za lazima. Kwa hiyo nawataka makamanda wote msimamie hili kwa dhati na kwa nguvu zenu zote.
Pia lipo suala la ajali za barabarani ambalo limekuwa likikua siku hadi siku hasa ajali zinazohusisha pikipiki maarufu kama boda boda. Ninaunga mkono harakati zinazofanywa na kitengo cha usalama barabarani katika kutoa elimu ya usalama barabarani, lakini nawataka nguvu kubwa pia ielekezwe huko kama mlivyoelekeza nguvu kubwa kukabiliana na ajali za barabara kwa mabasi na malori yaendayo mikoani. Kwa mfano kwa Jiji la Dar es Salaam pekee, karibu kila siku kumekuwa kukiripotiwa ajali zinazohusisha bodaboda na nyingi zinasababisha vifo au ulemavu kwa madereva na hata abiria wao na wakati mwingine hata kwa watumiaji wengine wa barabara. Ajali hizi zidhibitiwe.
Mbali na kuhusika katika ajali za barabarani, bodaboda pia zimekuwa zikihusika sana katika matukio ya kihalifu hasa unyang’anyi wa kutumia silaha. Ni rai yangu kwenu kuwa baada ya mkutano huu mtoke na suluhisho kwa tatizo hili hasa uhalifu wa kutumia silaha kwa kutumia pikipiki jijini Dar es salaam.
Ndugu Wajumbe,
Yapo malalamiko kadhaa juu ya baadhi ya askari na maafisa wachache wanaotumia beji ya polisi vibaya kwa kuwabambikia kesi wananchi, kuomba na kupokea rushwa, kuchelewa kufika eneo la tukio hata kama ni umbali mfupi tu, kula njama na watuhumiwa na hivyo kuharibu vielelezo vya kesi, kuchelewesha upelelezi wa kesi, kutokuwajali wateja (huduma bora kwa mteja) na mengi mengineyo ambayo yamekuwa ni kero kubwa sana kwa jamii. Natambua kuwa mmekuwa mkiwashughulikia askari na maofisa waliotuhumiwa kujihusisha na tabia hizi kwa mujibu wa sheria, lakini nitoe rai kwenu viongozi kuongeza jitihada zaidi katika kushughulikia matatizo haya kwa kuwasimamia ipasavyo askari wenu kuanzia ngazi ya chini kabisa. Nawahakikishia kuwa Serikali haitafumbia macho askari au Afisa yeyote atakayefanya mambo haya ya hovyo bila kujali cheo chake. Tutachukua hatua kwa faida ya Watanzania.
Ninaimani kuwa kila kiongozi akijiepusha katika kulinda na uendekeza mambo ya hovyo na akiwasimamia anaowaongoza ipasavyo na kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi na za nchi, malalamiko ya aina hiyo yatapungua sana kama si kumalizika kabisa.
Ndugu Wajumbe,
Mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu ndiyo jjukumu la msingi la Jeshi la Polisi. Ninawataka makamanda wote wa mikoa kuweka mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu katika himaya zenu ili kupunguza uwezekano wa wahalifu kukimbilia maeneo mengine pindi wanapofanya uhalifu. Aidha mafunzo kazini yaimarishwe ili kuwajengea askari uwezo wa kukabiliana nauhalifu.
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni jukumu la kila mmoja wenu, tunasikia taarifa za kukamatwa mirungi na bangi kwa wingi lakini dawa za kulevya za viwandani hatuzikii zikikamatwa. Nawakumbusha kudhibiti mitandao ya madawa ya kulevya ya viwandani. Tutapima ufanisi wenu kwa kuangalia uhalifu wa aina zote hasa eneo hili la madawa ya kulevya. Ni wazi kuwa hii ni vita kubwa na inahitaji umakini wa hali ya juu katika kukabiliana nayo kutokana na namna biashara hii inavyoendeshwa. Ninawasihi katika mkutano huu mtoke na mkakati wa namna ya kushughulika na wote wanaojihusisha na biashara hii haramu ili kuikomesha kabisa.
Ndugu wajumbe,
Kwa kumalizia niseme tena kuwa ni matumaini yangu kikao hiki kitaleta tija kwa taifa zima na maazimio mtakayotoka nayo ndiyo yatakuwa dira katika njia mtakayopita mwaka huu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku na kuhakikisha kuwa amani tuliyonayo inadumishwa.
Ndugu IGP, Makamanda na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi,
Mwisho ingawa si mwisho kwa umuhimu, natumia nafasi hii kuwapongeza Makamishna Albert Nyamhanga, Nsato Marijani na Simon Sirro kwa kupandishwa vyeo na kupewa nafasi za juu za kuwatumikia Watanzania mkiwa Makamishna wa Polisi. Nafasi hizo ni mzigo mzito kwenu. Nawatakia kila la kheri katika utumishi wetu. Nitoe tena shukrani za dhati kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kunialika kusema nanyi na kufungua Kikao hiki muhimu.
Baada ya kusema hayo sasa ninatamka rasmi kuwa kikao kazi cha Maafisa Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa polisi wa Mikoa na Vikosi cha Mwaka 2016 kimefunguliwa rasmi.
ASANTE SANA KWA KUNISIKILIZA
(Imechotwa katika mtandao wa Page not found | Ministry of Home Affairs

10. Uandishi wa Risala
Maana ya risala
Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa maelezo ya haja zao mbalimbali na mahitaji yao au kuonesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.Muundo wa risala

Utangulizi

· Cheo cha kiongozi anayehusika
· Kundi linalowakilishwa

Kiini
· Maelezo ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi linalowakilishwa.
· Mapendekezso na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.

Hitimisho
· Huwa na shukrani, msimamo pamoja na hitimisho.

Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni hotuba fupi lakini inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe huwa ni maelezo ya muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika hotuba. Utungaji wa risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo wazi kueleweka kwa kiongozi.

Mfano wa risala:

Ndugu Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa shuleni.

Shukrani zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema; kwasababu tupo tofauti sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.

Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47. Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu kidato cha nne.

Ndugu mgeni rasmi, elimu hii ya kidato cha nne imetupatia msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo mbalimbali kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla, pia tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa, usalama katika mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda. Vilevile tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa taifa.

Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.

Ndugu mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama ifuatavyo;

Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).

Ndugu mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii inapelekea kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.

Ndugu mgeni rasmi, maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.

Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote tunayocheza hapa shuleni.

Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa.

Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.

Mwisho tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.

Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.

11. Uandishi wa Mdahalo
Mdahalo ni majibizano yenye utaratibu maalumu. Ni kichocheo cha utafiti na njia ya kuelimishana. Mdahalo hufanywa kwa mashindano, ambapo upande mmoja hutoa hoja za kutetea jambo linalozungumziwa na upande mwingine hutoa hoja za kupinga. Kila upande hujitahidi kutetea msimamo wake mpaka mwisho.

Katika mdahalo, kunaweza kuwepo watu wa kati ambao hawafungamani na upande wowote. Hawa huweza kutetea upande fulani wakati fulani na kupinga uande huo huo wakati mwingine.
Mdahalo hugawanyika katika sehemu kuu tatu:
Utangulizi: huwa na maneno ya kuvuta makini ya wasikilizaji na ndimo ufafanuzi wa mdahalo hutolewa kwa ufupi.
Mdahalo wenyewe: katika sehemu hii, mzungumzaji huonesha msimamo wake kuhusu mada ya mdahalo, hutoa hoja za kutetea msimamo wake kwa kutoa hoja zenye ushahidi na mifano.
Hitimisho: huwa na muhtasari wa mawazo makuu ya mdahalo. Mzungumzaji huonesha msimamo wake kwa kutumia lugha ya kuvuta wasikilizaji.

Mambo ya kuzingatia katika kufanya mdahalo
· Mzungumzaji anapaswa kuelewa mdahalo kabla ya kuanza kupinga au kuetetea.
· Mzungumzaji apange na kuandaa hoja zake za kutetea au kupinga mdahalo. Hoja hizo zinaweza kuandikiwa maelezo mafupi.
· Katika hoja za mzungumzaji, achague zilizo nzito zaidi na awe mwangalifu asichague hoja zisizohusiana na mada.
· Mzungumzaji asikilize kwa makini hoja za wengine na kati ya hizo achague anazokubaliana nazo.
· Hoja zote zipangwe kimantiki na ziwasilishwe kwa kuzingatia lafudhi sahihi na uteuzi mzuri wa maneno.
· Mzungumzaji atumie lugha ya kimazungumzo katika uwasilishaji wake.
Kwa nini tunafanya midahalo?
Kwa kujitayarisha na kushiriki katika midahalo wanafunzi wanajifunza kutumia taarifa kuunga mkono hoja zao. Wanajifunza namna ya kuwasilisha mawazo yao kwa uwazi na kwa ushawishi mkubwa.
Kwa kushiriki katika midahalo, wanajifunza kuelewa mawazo ambayo ni tofauti na yao kwa sababu, wakati wa kufanya mdahalo, wanaweza kujadiliana kwa kutoa hoja kwa jambo ambalo hawakubaliani nalo kikamilifu, na wanapaswa kuelewa mawazo ya wenzao wa timu ya wasiokubali hoja zao.
Matayarisho ya mdahalo
Wafanya midahalo wazuri hujitayarisha vizuri. Mdahalo unaofanywa darasani unaweza usiwe rasmi, lakini unaweza kuwajenga wanafunzi katika hali inayowafanya wanafunzi wafanye mdahalo rasmi katika mashindano.
Kabla ya kuandaa mdahalo, wafanya midahalo wanakusanya taarifa nyingi kwa kadri iwezekanavyo, kutoka katika maktaba, magazetini, na kwa kujadiliana na watu.
Wanafikiria hoja zote zinazounga mkono mada yao, na zile zinazopinga hoja yao. Kwa maana nyingine ni kuwa, wanaelewa hoja za wapinzani wao pamoja na hoja zao. Wanajitayarisha kwa maswali yoyote wanayoweza kuulizwa na wapinzani wao, na changamoto zozote zinazoweza kutolewa.
Wafanya midahalo wazuri hutayarisha hoja zao katika muundo mzuri wa ushawishi. Wanawasikiliza watu wengine wanaofanya mdahalo, ili wajifunze ufundi na stadi za kufanya mdahalo. Wanajiunga na vyama vya kufanya midahalo, na kufanya midahalo mara kwa mara.
Mchakato wa mdahalo
Kuna timu mbili, kila timu ina wazungumzaji wawili au watatu. Timu moja (chanya) inaafiki hoja, na timu nyingine (hasi) inapinga hoja.
Kuna mwenyekiti, ambaye anaendesha utaratibu.
Mdahalo na muda wa mdahalo huo unagawanywa sawasawa kwa timu zote mbili.
Kila mzungumzaji anatoa mdahalo kama upande wake umeandaa kuunga mkono hoja zao. Pande zinazungumza kwa zamu, wakianza na anayependekeza hoja (chanya, hasi, chanya, hasi). Kila mzungumzaji ana muda maalum wa kuzungumza (k.m. dakika tatu au tano)
Baadaye mdahalo unaweza kufunguliwa kwa washiriki wengine, kwa wasemaji kusimama na kutoa hoja zao za kuunga mkono au kupinga mada ya mdahalo. Kila mzungumzaji kutoka upande wa wasikilizaji anapewa muda maalum wa kuzungumza ( k.m. dakika moja au dakika tatu).
Kila timu inaweza pia kuzungumza kwa kujibu hoja za wapinzani wao, baada ya kila timu kupewa muda kidogo wa mashauriano. Hii ina maana kuwa wana nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wapinzani wao. Kila timu inaweza kupewa nafasi ya kupinga hoja dhidi ya hoja zilizotolewa na wenzao mara moja au zaidi. Nafasi ya kwanza ya kupinga hoja wanapewa wale wanaopinga mjadala na nafasi ya mwisho inatolewa kwa wanaounga mkono mjadala.
Kanuni muhimu za mdahalo
Timu inayounga mkono mjadala haitakiwi kubadili hoja zao. Aidha, ile inayopinga mjadala nayo pia hairuhusiwi kubadili hoja zao. Wanapaswa kupinga kabisa mjadala licha ya maoni yao binafsi.
Ikiwa mzungumzaji anatoa tamko, wanatakiwa kutoa ushahidi au sababu za kuunga mkono tamko hilo.
Taarifa zinazotolewa katika mdahalo lazima ziwe sahihi.
Wazungumzaji hawaruhusiwi kuleta hoja mpya wakati wa kujibu/kupinga hoja za wenzao.
Hoja ya utaratibu na hoja ya taarifa
Yeyote anayehusika na mdahalo anaweza kuingilia kati wakati msemaji akizungumza kwa kunyoosha mikono na kusema kuwa ‘anataka kutoa hoja’. (Hii ni ‘hoja ya utaratibu’). Hii ina maana kuwa anataka kueleza kuwa moja ya kanuni za mdahalo imevunjwa (k.m. mzungumzaji amezidisha muda wake wa maongezi, au hana ushahidi wa kuthibitisha hoja zake).
Wana-mdahalo wanaweza pia kunyoosha mikono yao wakitaka kutoa ‘hoja ya taarifa’ (swali au taarifa za ziada wanazoweza kutoa). Msemaji anaweza kuamua kumruhusu mshiriki kuzungumza, lakini halazimiki.
Uamuzi
Timu inayoshinda katika mdahalo inaamuliwa na jaji au majaji kwa kutegemea ubora wa mjadala.
Aidha inaweza pia kuamuliwa kwa kupigiwa kura.
Mfano wa mdahalo
Asante Mwenyekiti,katibu,mtunza muda na washiriki wote. Nipo mbele yenu kuunga mkono mada isemayo Pesa ni chanzo cha maovu yote kwa hoja zifuatazo.
Hoja ya kwanza,………
Hoja ya pili,………
Hoja ya tatu,………..
Hoja ya nne,………..
Hoja ya tano,……..
Kwa hoja hizo nahitimisha kwa kusema kuwa ni kweli kabisa kuwa pesa ndio chanzo cha maovu yote kwa wanadamu.

12. Taarifa za kikao
Kumbukumbu za kikao ni muhtasari wa mambo yaliyojadiliwa na kukubaliwa katika kikao. Ni muhimu kuandika kumbukumbu za kikao ili kusaidia na kurahisisha utekelezaji wa mambo yaliyoamuliwa. Pia kumbukumbu za kikao hutumika kwa ajili ya marejeleo kwa vizazi vya baadaye.Namna ya kuandika kumbukumbu za kikao
Katika kuandika kumbukumbu mwandishi hana budi kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Kichwa cha kumbukumbu
Kichwa cha kumbukumbu kioneshe kuwa kikao kinahusu nini, kilifanyikia wapi na tarehe gani.

(b) Mahudhurio
Mwandishi anapaswa kuandika orodha ya majina ya watu waliohudhuria kikao na wasiohudhuria. Kama kikao kinahudhuriwa kwa mara ya kwanza mahudhurio yatakuwa na majina ya waliohudhuria tu.

© Uteuzi wa viongozi
Iwapo kikao kinahudhuriwa kwa mara ya kwanza wajumbe hupaswa kuteua viongozi wa kikao hicho ambao ni Mwenyekiti na Katibu kabla ya kuanza kwa kikao. Kikao hakiwezi kuanza pasipo viongozi wa kusimamia mijadala yote katika kikao husika.

(d) Ufunguzi wa kikao
Baada ya kuteua viongozi, Mwenyekiti aliyeteuliwa hufungua kikao rasmi na kuanzisha mijadala ya kikao cha siku hiyo na siku zijazo hadi itakapokuwa vinginevyo

(e) Ajenda
Hapa huandikwa ajenda zilizojadiliwa kwenye kikao. Mambo yaliyojadiliwa katika kila ajenda yaandikwe kwa muhtasari. Kwa kila ajenda kauli ya kukubaliwa au kukataliwa itamkwe wazi.

(f ) Mengineyo
Hapa huandikwa ajenda ambazo hujitokeza katika kikao lakini hazikupitia kwa Mwenyekiti na zinastahili kujadiliwa kama ajenda.
(g) Yatokanayo
Hapa huandikwa mambo ambayo yamejitokeza katika kikao na hayana uhusiano na ajenda za kikao. Kwa mfano masuala mtambuka kama mjumbe kulipia gharama za kikao,taarifa ya dharura inayoweza kumfanya mjumbe aondoke kabla ya kikao kuahirishwa, n.k

(h) Kuahirisha kikao
Baada ya majadiliano ya ajenda, Mwenyekiti huahirisha kikao. Mwandishi wa kumbukumbu azingatie muda kikao kilipoahirishwa.

Baada ya kikao mwandishi apitie tena kumbukumbu hizo na aziandike vizuri na kuzihifadhi kwa ajili ya marejeleo ya kikao kijacho. Kumbukumbu hizo zitiwe saini na Mwenyekiti na Mwandishi (katibu) kisha wakati wa mkutano mwingine zisambazwe na kusomwa na wajumbe wa mkutano. Baadaye zithibitishwe na wajumbe na Mwenyekiti na atie saini ya kuthibitishwa huko.

Ufuatao ni mfano wa kumbukumbu za kikao kinachofanywa kwa mara ya kwanza:

KUMBUKUMBU ZA KIKAO CHA KWANZA CHA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO KUHUSU MAHAFALI KILICHOFANYIKA TAREHE 5/4/2017 KATIKA UKUMBI WA SHULE KUANZIA SAA 4:00 ASUBUHI HADI SAA 6:00 MCHANA.

(a) Mahudhurio
Waliohudhuria (orodhesha majina yao)
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Wasiohudhuria (orodhesha majina yao)
-
-
-
-
-
-
-
-
-
(b) Uteuzi wa viongozi
Kiranja wa darasa aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kikao na katibu wake ni kiranja msaidizi. Wajumbe wote walikubaliana na uteuzi huo.


© Kufungua kikao
Kiranja wa darasa ambaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kikao hicho alifungua kikao mnamo saa 4:00 asubuhi kwa kuwaeleza wajumbe madhumuni ya kikao hicho.

(d) Ajenda
- Siku na mahali pa mahafali
- Mgeni rasmi
- Zawadi
- Michango ya sherehe
- Uteuzi wa kamati

Siku na mahali pa mahafali
Wajumbe walijadiliana na kukubaliana kwa pamoja kuwa mahafali yafanyike jumamosi ya pili kabla ya kuanza kwa mitihani ya kitaifa ili kuwawezesha waalikwa wote kuhudhuria lakini pia kutoa muda wa kutosha kwa wahitimu kujiandaa kwa mitihani yao.Kuhusu mgeni rasmi
Wajumbe walikubaliana kuwa jukumu la kutafuta mgeni rasmi apewe mkuu wa shule.

Kuhusu zawadi
Wajumbe walijadiliana na kukubaliana kuwa zawadi zitapangwa na kuamuliwa na kamati itakayoundwa.

Michango ya sherehe
Kikao kiliazimia kwa pamoja kuwa ili kupata pesa za kufanikishia mahafali kila mjumbe apewe fomu maalumu itakayoandaliwa ili kuchangisha toka kwa ndugu, jamaa na marafiki kiasi chochote atakachoguswa mtu kuchangia.

Uteuzi wa kamati
Wanafunzi wafuatao walichaguliwa ili wafanye mipango ya kuandaa na kusimamia sherehe ya mahafali yao. Wanafunzi hao ni;

- Mtungi
- Baraka
- Mujuni
- Byoma
- Shukuru
- Sikudhani
- Kachacha
- Stumai
- Tamasha
- Kaitaba
Wajumbe hao walikubaliana na uteuzi huo na wakaahidi kupeana majukumu.


(f) Mengineyo
Wajumbe walisisitiza kwamba kamati ifanye mipango kwa kuzingatia kwamba muda uliobaki ni mfupi. Walipendekeza kwamba kufanyike mkutano wa kuwapatia wajumbe taarifa kuhusu mgawanyo wa majukumu.

(g) Yatokanayo
Mjumbe mmoja aliwaburudisha wajumbe kwa vinywaji na nyama choma ya mbuzi katika kumbukumbu yake ya kuzaliwa.

(h) Kuahirisha kikao
Mwenyekiti aliahirisha kikao kwa kuwaomba wajumbe wengine wawe na ushirikiano kwa wenzao katika kufanikisha mahafali hayo. Kikao liahirishwa saa 6:00 mchana. Kikao kijacho kitakuwa 12/4/2017 kuanzia saa 9:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.

Mwenyekiti…………………….Tarehe…………………………........ Katibu………………………….Tarehe……………………………….

Ikiwa kikao kinafanyika kwa mara ya pili:

Kikao cha pili na kuendelea huwa na muundo ufuatao:
1. Kichwa cha kikao
2. Mahudhurio
3. Kusomwa na Kuthibitishwa taarifa za kikao kilichotangulia
4. Kufungua kikao
5. Ajenda
6. Mengineyo
7. Yatokanayo
8. Kuahirisha kikao
9. Majina & saini za viongozi
13. UANDISHI WA RIPOTI
Ripoti ni maelezo kuhusu mtu, kitu au jambo fulani lililotokea. Ni aina ya kumbukumbu ambazo huandikwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Ripoti inaweza kuwa ya uchunguzi wa utafiti kuhusu jambo fulani, inaweza kuwa ya polisi, daktari au ya tume fulani.


Namna ya kuandika ripoti

Kabla ya kuandika ripoti lazima kuwe na ushahidi unaohusu suala au jambo linaloandikiwa ripoti hiyo. Kwa hiyo, ni lazima mtunzi afanye uchunguzi kwanza. Pia mtunzi anapaswa kufahamu kiwango cha elimu na uwanja wa mtu anayemwandikia ripoti hiyo. Kwa mfano kama ni polisi, daktari, mwanasheria, mfanyabiashara n.k. Lugha atakayoitumia mwandishi au mtunzi izingatie muktadha wa matumizi. Lugha itegemee aina ya ripoti.


Hatua za uandishi wa ripoti


(a) Kichwa cha ripoti
Mtunzi aandike kichwa cha ripoti ambacho kinaonesha; kiini cha ripoti- ripoti inahusu nini, tarehe ya tukio au jambo linaloandikiwa ripoti na mahali palipotokea jambo hilo.


(b) Utangulizi wa ripoti
Katika hatua hii mtunzi hueleza kwa muhtasari madhumuni ya ripoti


© Kiini cha ripoti
Mtunzi aeleze mambo aliyoyaona, chanzo chake na madhara au faida yake


(d) Hitimisho
Katika kuhitimisha ripoti mtunzi aoneshe msimamo na mapendekezo yake. Baada ya hitimisho mtunzi aandike au aoneshe ripoti imeandikwa na nani, cheo chake (nafasi yake hasa katika ripoti hiyo) na tarehe ripoti hiyo ilipoandikwa.


Ufuatao ni mfano wa ripoti ya mkutano wa wanafunzi

Ripoti ya kikao cha wanafunzi wa kidato cha tano uliofanyika katika ukumbi wa shule mnamo tarehe 10/4/2017 kuhusu mahafali yao.


Mnamo tarehe 10/4/2017 saa 4:00 asubuhi, wanafunzi wa kidato cha tano walifanya mkutano kuhusu mahafali yao yatakayofanyika mwezi Mei mwaka huu.


Mambo yaliyojadiliwa siku hiyo ni pamoja na :

(i) Kuwakaribisha wazazi wao
(ii) Kuandaa michezo mbalimbali: mpira wa miguu, mpira wa
kikapu, ngonjera, nyimbo, igizo, mashairi na muziki.
(iii) Kuandaa zawadi kwa ajili ya walimu wao wa madarasa, wa
masomo na Mkuu wa shule.
(iv) Kutoa mchango wa kununulia zawadi hizo.


Wanafunzi walitoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kumwomba kiranja wao wa darasa awaeleze walimu kwamba siku hiyo wanafunzi wanaomba wasivae sare za shule na pia waruhusiwe kuwakaribisha wanafunzi wa shule nyingine kwa ajili ya kucheza nao dansi na wakati wa muziki pawekwe ulinzi mkali ili wasiingiliwe na watu wa nje.


Mwisho wanafunzi wote walikubaliana kuchanga Tshs. 2000/= kila mmoja ili kufanikisha shughuli hiyo.


Mkutano huo uliodumu kwa saa mbili ulifungwa saa 6:00 mchana na kiranja wa darasa.


Imetayarishwa na. Saini………………………..
Jina………………………...


Tarehe………………... Cheo…………………….....14. Uandishi wa Wasifu
Wasifu ni insha inayosimulia maisha ya mtu fulani tangu kuzaliwa kwake, elimu yake, kazi, ujuzi wake n.k. Anayeandika wasifu ni tofauti na anayezungumziwa katika wasifu huo.

Kuna aina tatu za wasifu:
Wasifu wa Kawaida
Tawasifu/Wasifu binafsi
Wasifu-Kazi

Wasifu wa kawaida.
Wasifu wa kawaida ni masimulizi y
07-14-2017 06:42 AM
Visit this user's website Find all posts by this user Like Post Quote this message in a reply
Post Reply 


You may also like these discussions:
Thread: Author Replies: Views: Last Post
  Uandishi MyElimu 0 394 12-04-2017 02:45 PM
Last Post: MyElimu
Post Icon Uandishi Wa Barua MyElimu 0 829 10-19-2017 07:21 PM
Last Post: MyElimu
  Uandishi Wa Insha MyElimu 0 952 10-19-2017 07:11 PM
Last Post: MyElimuUser(s) browsing this thread: 1 Guest(s)